Balozi wa Tanzania nchini China asema, uhusiano kati ya China na Tanzania ni zaidi ya wa jadi, ni wa kindugu

By Aris (Tovuti ya Gazeti la Umma) April 25, 2024

Balozi wa Tanzania nchini China Khamisi Mussa Omar amesema katika mahojiano na gazeti la People’s Daily Online yaliyofanyika hivi karibuni ofisini kwake mjini Beijing kwamba, uhusiano wa China na Tanzania ni zaidi ya ule wa jadi kwani ni uhusiano wa kindugu wenye historia ya muda mrefu inayoanzia kabla ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujipatia uhuru wake.

Katika mahojiano hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yameangazia uhusiano wa China na Tanzania unapoelekea kutimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake, Balozi Omar amesema, kabla ya Tanzania, uhusiano kati ya China na Tanganyika ulianza tarehe 9, Desemba, 1961 siku ya uhuru wa Tanganyika, na kwa Zanzibar ulianza baada ya mapinduzi, lakini baada ya Muungano na kuundwa kwa Jamhuri moja ya Tanzania, mwaka 1964, China haraka sana ilianzisha uhusiano wa kibalozi na kidiplomasia na Tanzania.

Balozi wa Tanzania nchini China, Khamisi Mussa Omar akionekana kwenye picha baada ya mahojiano na  People’s Daily Online yaliyofanyika Tarehe 16, Aprili kwenye Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, Beijing. (Mpiga picha: Zhoulinjia/People’s Daily Online)

Balozi wa Tanzania nchini China, Khamisi Mussa Omar akionekana kwenye picha baada ya mahojiano na People’s Daily Online yaliyofanyika Tarehe 16, Aprili kwenye Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, Beijing. (Mpiga picha: Zhoulinjia/People’s Daily Online)

Amesema, kabla ya uhuru wa Tanganyika na mapinduzi ya Zanzibar, China na Tanzania vilevile zilishaanzisha uhusiano wakati wa kutafuta uhuru.

“Takribani marais wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walipata nafasi ya kutembelea China katika kipindi chao…...na viongozi wa China vilevile wametembelea Tanzania. Kwahiyo uhusiano ni wa kindugu, umeendelea kupanuka, hadi umefikia ngazi ya ushirikiano wa washirika wa kimkakati wa pande zote” amesema.

Ameeleza kuwa katika miaka yote hiyo, Tanzania na China zimekuwa na uhusiano ulioimarika na thabiti, zikishirikiana katika siasa, stratejia za kijeshi, uchumi, biashara, uwekezaji, jamii, utamaduni na kadhalika. Amesema, uhusiano ni mzuri na anategemea utaendelea kuwa hivyo.

Balozi Omar ametaja kwa kusifu miradi ya kihistoria ya ushirikiano kati ya China na Tanzania ukiwemo ule wa reli ya TAZARA yenye urefu wa Kilomita 1860 inayoanzia Dar es Salaam, Tanzania hadi Kapilimposhi, Zambia, ambayo mchakato wake ulianza miaka ya 1960 hadi kuja kukamilika kwa kuzinduliwa kwake Mwaka 1976. “Huu ndiyo unakumbukwa zaidi kwa ukubwa wake” amesema.

Amesisitiza kuwa, katika miaka ya nyuma na hadi sasa miradi mingi sana imetekelezwa, karibu kwenye sekta zote hususan kwenye uwekezaji wa viwanda hasa kiwanda cha kihistoria cha URAFIKI, kilimo, mawasiliano, michezo hasa ujenzi wa uwanja mkubwa wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam na ukarabati wa ule wa Abeid Karume, upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam huku miradi mingine mingi kama ile ya barabara kwa sehemu kubwa ikiwa imejengwa na kampuni za China.

Balozi Omar ametaja pia mabadilishano kati ya watu, ya kitamaduni na yale ya teknolojia na ujuzi kama sehemu nyingine iliyopata mafanikio.

Kuhusu eneo hili la mabadilishano, Balozi Omar amesifu sana timu za madaktari wa China kutoka mikoa ya Jiangsu na Guangdong ambazo zimekuwa zikitoa usaidizi wa matibabu kwa Zanzibar na Tanzania Bara, mtawalia kwa miaka mingi sana.

Amesema kuwa, katika mabadilishano ya ujuzi na teknolojia, kuna watanzania wengi sana wanakuja kusoma China.

“Katika miaka ya karibuni baada ya kugundua ubora wa elimu ya China unaendelea kuongezeka watanzania wengi sana wamechagua kuja China kusoma, kabla ya UVIKO-19 kuna wakati walifikia 5000” amesema Balozi Omar huku akisisitiza kuwa angependa kuona eneo hili la mabadilishano ya kielimu likijikita zaidi katika teknolojia, ujuzi na maarifa mahsusi yanayohitajika katika sekta lengwa na uongezaji thamani ya malighafi na mazao ili kuendeleza sekta ya viwanda na mauzo ya nje ya Tanzania.

Ameeleza kuwa, katika kuendeleza mabadilishano zaidi kati ya pande hizo mbili, viongozi wakuu wa China na Tanzania walipokutana Mwaka 2022 walikukubaliana kuwa Mwaka 2024 utakuwa Mwaka wa Utamaduni na Utalii wa China na Tanzania.

Amesema, ubalozi wa Tanzania utafanya shughuli za uzinduzi wa mwaka huo mjini Beijing, China, tarehe 15 Mei kwa kushirikiana na upande wa China ambapo kutakuwa na ushiriki wa wasanii kutoka Tanzania, na shughuli mbalimbmali za kutangaza utalii katika baadhi ya maeneo nchini China zitafanyika.

Mwaka huu ni mwaka ambao Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), linatazamia kufanya mkutano wake wa kilele utakaokutanisha viongozi wakuu wa Afrika na China mjini Beijing. Balozi Omar amesema, jukwaa hilo ni muhimu kwa Afrika, ni muhimu kwa China vilevile.

“Linaleta pamoja watu bilioni 1.4 wa Afrika na wenzao bilioni 1.4 wa China. Kwahiyo ukitazama FOCAC inacholeta ni watu bilioni 2.8 wa Dunia kwenye jukwaa moja” amesema Omar, huku akiongeza kuwa, jukwaa hilo limekuwa ni kwa ajili ya ushirikiano na kuleta maendeleo ambayo yanasaidia pande zote mbili hususan Afrika inayokabiliwa na pengo la teknolojia, sekta ya viwanda ambayo bado haijaendelea, ukosefu wa nguvu kazi zenye ujuzi, miundombinu isiyo toshelezi, hitaji la ajira kwa kundi la vijana na changamoto nyinginezo.

Amesema, katika mkutano huo, Rais Xi Jinping wa China atapata fursa ya kukutana na viongozi wa Afrika ili kuzungumzia miaka mitatu minne inayokuja, na tayari vikao vya maandalizi, kwa kutazama hasa mwelekeo wa pande zote mbili na maeneo ambayo yana maslahi ya pande zote mbili yameshaanza.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha