Zambia yajitahidi kutokomeza malaria kwa msaada wa China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 25, 2024

LUSAKA – Zambia ingependa kujifunza kutoka kwenye mafanikio ya China katika kutokomeza malaria ili kuharakisha kasi yake ya kupambana na ugonjwa huo, Sampa Chitambala-Otiono, kaimu mkurugenzi wa Kituo cha Taifa cha Kutokomeza Malaria cha Zambia amesema siku ya Jumatano.

Otiono amesisitiza umuhimu wa kujifunza kutoka kwenye uzoefu wa China wakati Zambia inapojitahidi kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030.

"Hali nchini China inaweza kuwa tofauti, lakini nina uhakika kwamba kuna jambo moja au mawili tunaweza kujifunza kutoka China ili kuongeza kasi ya kutokomeza malaria," amesema.

Afisa huyo ameishukuru China kwa kuunga mkono mapambano dhidi ya malaria kwa miaka mingi, akisema China imetoa uungaji mkono wa kutosha kama vile kutoa magari kwa mpango wa malaria, msaada wa vifaa vya maabara pamoja na kufanya programu za mafunzo.

Amesema, malaria inaendelea kuwa suala kubwa la afya ya umma nchini humo, ikichukua asilimia 30 ya magonjwa, licha ya hatua za kuingilia kati ambazo zimetekelezwa.

Zambia inalenga kuanza kutumia chanjo dhidi ya malaria mwaka ujao, amesema, huku akiongeza kuwa nchi hiyo itahitaji kuchambua ufanisi wa chanjo hiyo na madhara yake kabla ya kuwachanja watu.

Amesema changamoto kubwa ya Malaria nchini humo inatokana na sababu mbalimbali, ikiwamo tabianchi inayoweka mazingira mazuri ya kuzaliana kwa mbu, pamoja na masuala mbalimbali kama vile kutofuata mbinu dhidi ya malaria za matumizi ya mara kwa mara ya vyandarua vyenye viuatilifu. Zaidi ya hayo, umbali mrefu wa vituo vya afya na ukosefu wa uzalishaji wa ndani wa dawa vimetajwa pia zinasababisha hali suala hilo.

Amesema wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ndiyo wanaoathirika zaidi na malaria na kwamba serikali ya Zambia inahakikisha kuwa makundi haya mawili yanapata kipaumbele katika upatikanaji wa huduma za kukabiliana na malaria.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha