

Lugha Nyingine
Kenya yasema juhudi zinaendelea kurejesha intaneti katika eneo la Afrika Mashariki baada ya kukatika kwa kebo za baharini
NAIROBI - Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CA) imesema Jumatatu kuwa juhudi zinaendelea kurejesha huduma za intaneti ambazo zimetatizika kote Afrika Mashariki.
Mamlaka hiyo imethibitisha kuwa kukatika kwa nyaya za intaneti kwenye bahari kuu kumetokea siku ya Jumapili katika kituo cha mawasiliano cha Mtunzini nchini Afrika Kusini, kukiathiri kebo kadhaa za mkongo wa intaneti zinazohudumia Kenya, ikiwa ni pamoja na Mfumo wa Kebo wa Chini ya Bahari wa Afrika Mashariki (EASSy) na kebo za Seacom.
"Tunapenda kuwafahamisha wateja binafsi na kampuni kuwa mchakato wa kurejesha huduma umeanza, lakini kutatizika kwa intaneti na kasi ndogo huenda vikaendelea katika siku chache zijazo kabla ya huduma kurejeshwa kikamilifu," Mkurugenzi Mkuu wa CA David Mugonyi amesema katika taarifa iliyotolewa Nairobi, Kenya.
Mugonyi ameagiza watoa huduma kuchukua hatua za mapema ili kupata njia mbadala za mpitisho wa mawasiliano yao na anafuatilia hali hiyo kwa karibu ili kuhakikisha kuwa muunganisho wa intaneti unaoingia na kutoka unapatikana.
Bw. Ben Roberts, ofisa mkuu wa teknolojia na uvumbuzi katika kundi la utoaji huduma ya mtandao la Liquid Intelligent Technologies, amesema, kukatika kwa kebo mbili za mkongo wa intaneti zinazounganisha Kenya na Afrika Kusini kumeathiri vibaya huduma za intaneti katika nchi za Afrika Mashariki.
Ben ameongeza kuwa kebo tatu muhimu za mkongo katika Bahari Nyekundu, Seacom, Europe India Gateway (EIG), na Asia-Africa-Europe 1 (AAE-1), pia zimekatika na kubaki bila kukarabatiwa, na kusababisha kukatika kwa intaneti.
Chanzo cha mara moja cha hitilafu hizo, ambazo zinaripotiwa kuathiri mifumo ya kebo za Eassy na Seacom zinazotumika katika pwani ya mashariki mwa Afrika, hakikuweza kujulikana.
Mwezi Machi, mwamba unaoshukiwa kuwa chini ya maji uliteleza kwenye ufukwe wa Cote d'Ivoire, na kusababisha kebo kadhaa za mkongo wa intaneti wa baharini kupoteza mawasiliano.
Hitilafu hiyo iliathiri nchi 13 za Afrika zilizo katika ufukwe wa bahari wa Afrika Magharibi, na kusababisha huduma kutatizika au karibia kukatika kwa intaneti.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma