FAO yaeleza wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa matumizi ya dawa za kuwaua wadudu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 14, 2024

Lesedi Modo-Mmopelwa, mwakilishi msaidizi wa Shirika la Mpango wa Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), akizungumza kwenye hafla ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Afya ya Mimea huko Gaborone, Botswana, Mei 13, 2024. (Picha na Tshekiso Tebalo/Xinhua)

GABORONE - Shirika la Mpango wa Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) nchini Botswana limeelezea wasiwasi wake kwamba matumizi makubwa ya dawa za kuwaua wadudu ili kudhibiti wadudu, magugu na magonjwa yanaweza kuongeza hatari ya kudhuru viumbe muhimu kwa afya ya mfumo wa ikolojia.

Akizungumza kwenye hafla ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Afya ya Mimea huko Gaborone, mji mkuu wa Botswana, Jumatatu, Lesedi Modo-Mmopelwa, mwakilishi msaidizi wa FAO nchini humo, amesema karibu asilimia 40 ya mazao ya chakula yanapotea kila mwaka kutokana na wadudu, magugu na magonjwa.

"Hii siyo tu inaathiri uchumi lakini pia inaathiri kwa kiasi kikubwa usalama wa chakula na lishe nchini humo, hasa kwa makundi yaliyo hatarini katika jamii za vijijini ambazo kwa kiasi kikubwa zinategemea kilimo."

Kwa mujibu wa Modo-Mmopelwa, mabadiliko ya tabianchi na shughuli za binadamu pia zinaathiri afya ya mimea na kuharibu bioanuwai huku zikiweka mazingira mazuri kwa wadudu na magonjwa, na kusababisha wadudu hao kutokea katika maeneo ambayo hayakuwahi kuonekana hapo awali.

Amesisitiza kuwa matumizi ya dawa za kuwaua wadudu yanaweza kuongezeka kuenea kwa magonjwa, kuhatarisha vichavushaji, maadui wa asilia wa wadudu, na viumbe muhimu kwa mfumo wa afya wa ikolojia.

"Kwa hiyo ni muhimu kulinda afya ya mimea kwa kuvuka mipaka kwa kuhimiza ushirikiano wa kimataifa na viwango vya kimataifa, kama vile Viwango vya Kimataifa vya Hatua za Usafi wa Mimea," amesema.

Botswana inashirikiana na Mkataba wa Kimataifa wa Kulinda Mimea (IPPC), ambao unalenga kulinda mimea, mazao ya kilimo na maliasili dhidi ya wadudu waharibifu wa mimea duniani.

Umoja wa Mataifa uliweka Mei 12 kuwa Siku ya Kimataifa ya Afya ya Mimea. Ni siku iliyoandaliwa na Sekretarieti ya IPPC na FAO. Maadhimisho hayo ya mwaka huu yamefanyika chini ya kaulimbiu ya "Afya ya Mimea, Biashara Salama, na Teknolojia ya Kidijitali."

Mtu akiangalia sampuli chini ya darubini kwenye maabara wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Afya ya Mimea huko Gaborone, Botswana, Mei 13, 2024. (Picha na Tshekiso Tebalo/Xinhua)

Mtu akiangalia sampuli chini ya darubini kwenye maabara wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Afya ya Mimea huko Gaborone, Botswana, Mei 13, 2024. (Picha na Tshekiso Tebalo/Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha