China inapinga vikali Marekani kupandisha ushuru kwa bidhaa za China: Wizara ya Biashara ya China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 15, 2024

BEIJING - China inapinga vikali na kuwasilisha malalamiko juu ya ongezeko zaidi la ushuru wa ziada kwa baadhi ya bidhaa za China lililotangazwa na Marekani, na itachukua hatua kwa uthabiti kulinda haki na maslahi yake yenyewe, Wizara ya Biashara ya China imesema siku ya Jumanne.

Juu ya ushuru uliopo sasa chini ya Kifungu cha 301, Marekani imeamua siku ya Jumanne kuongeza ushuru wa ziada kwa uagizaji wake wa bidhaa za China ikiwa ni pamoja na magari yanayotumia umeme, betri za lithiamu-ioni, seli za jua, madini muhimu, semiconductors, chuma na aluminiamu, na kreni.

Msemaji wa Wizara ya Biashara ya China amesema katika taarifa kuwa, China inalaumu vikali Marekani kuzingatia hali ya siasa ya nchini humo na kutumia vibaya utaratibu wa mapitio ya ushuru wa Kifungu cha 301 kwa kuongeza ushuru wa ziada kwa baadhi ya bidhaa za China.

Hatua hii inayafanya masuala ya biashara yawe ya kisiasa na kuyatumia kama silaha, imesema taarifa hiyo, ikiielezea hali hiyo kuwa ni “mfano wazi wa uendeshaji wa kisiasa”.

Shirika la Biashara Duniani (WTO) tayari limeamua kwamba ushuru wa Kifungu cha 301 ni ukiukaji wa kanuni za WTO, lakini upande wa Marekani umeendelea na makosa yake, imesema taarifa hiyo.

Hatua hii ya Marekani ya kuongeza ushuru inakwenda kinyume na makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wa nchi mbili China na Marekani na ahadi za Rais wa Marekani Joe Biden, na kutaathiri vibaya hali ya ushirikiano baina ya nchi hizo mbili, imesema taarifa hiyo.

Upande wa Marekani unapaswa kurekebisha mara moja makosa yake na kuondoa hatua za ziada za ushuru dhidi ya China, imesema taarifa hiyo. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha