

Lugha Nyingine
Rais wa Ghana aitaka Afrika kuhamasisha teknolojia za mambo ya fedha, uchumi wa kidijitali kwa ajili ya mageuzi
Rais wa Ghana Nana Addo Dankwa Akufo-Addo (C) akishiriki katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kilele wa 3i wa Afrika mjini Accra, Ghana, Mei 13, 2024. (Picha na Seth/Xinhua)
ACCRA - Rais wa Ghana Nana Addo Dankwa Akufo-Addo siku ya Jumatatu akifungua Mkutano wa Kilele wa 3i wa Afrika katika mji mkuu wa Ghana, Accra amezitaka nchi za Afrika kuendeleza teknolojia za mambo ya fedha (fintech) na uchumi wa kidijitali ili kuharakisha kasi ya mageuzi.
Mkutano huo wa kilele wa siku tatu, wenye kaulimbiu ya "Kufungua Uwezo wa Kiuchumi wa Teknolojia za Mambo ya Fedha na Kidijitali wa Afrika," unalenga kuleta msukumo mkubwa na mvuto kwa ajenda ya Afrika ya mambo ya fedha ya kidijitali kwa kuunda jukwaa la mikutano kati ya mambo ya fedha, sera na teknolojia.
Akifungua mkutano huo, Akufo-Addo amezitaka nchi za Afrika kufanya miundombinu ya kidijitali kuwa uti wa mgongo wa ustawi wa watu wao, kukumbatia teknolojia zinazobadili uchumi wa dunia, na kuziunda kwa kuendana na mahitaji na changamoto za bara hilo.
Akufo-Addo amesema muundo mpya wa teknolojia za mambo ya fedha na uvumbuzi wa kidijitali utasaidia Waafrika kufaidika kwa kutosha na Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika (AfCFTA).
Ameongeza kuwa kwa kuwa AfCFTA ina uwezo wa kuchochea hali ya uchumi wa bara hilo na kuleta mageuzi, nchi za Afrika hazina budi kukumbatia mfumo wa kidijitali na teknolojia za mambo ya fedha ili kuendesha mageuzi hayo.
Kupitia ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi na ushirikiano wa kuvuka mpaka, mfumo mzuri na wenye ufanisi wa tenolojia za mambo ya fedha unaweza kuundwa ili kuendana na lengo la utandawazi wa uchumi wa Afrika, ameisema rais huyo wa Ghana.
"Kwa kufanya kazi kwa pamoja, tunaweza kufungua uwezo mkubwa wa nchi zetu na kuunda wimbi linaloinuka ambalo litainua boti zote kutoka miji midogo hadi miji mikubwa zaidi. Hili linawezekana pale tunapokumbatia mageuzi ya kidijitali."
Wamkele Mene, katibu mkuu wa Sekretarieti ya AfCFTA, amesema katika hotuba yake kwamba ujumuishwaji wa kidijitali ni muhimu kwa ajili ya kutumia kikamilifu uwezo mkubwa wa soko unaowakilishwa na watu bilioni 1.4 barani Afrika.
"Lakini kama tukifeli kuwezesha matumizi ya teknolojia hizi za kidijitali ambazo sote tutakuwa tukizijadili leo na kesho, itakuwa vigumu kwetu kufikia malengo yetu," Mene ameongeza.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma