Mazungumzo ya upatanishi nchini Kenya yalenga kuimarisha mchakato wa uchaguzi nchini Sudan Kusini

(CRI Online) Mei 15, 2024

Mazungumzo ya ngazi ya juu ya upatanishi wa Sudan Kusini, yanayoendelea mjini Nairobi, Kenya, yataongeza msukumo katika mchakato wa uchaguzi ujao nchini humo.

Hayo yamesemwa na mkuu wa kitivo cha masomo ya kijamii na kiuchumi katika Chuo Kikuu cha Juba cha Sudan Kusini Abraham Kuol Nyuon, huku akiongeza kuwa mazungumzo hayo yaliyofunguliwa Mei 3 na Rais William Ruto wa Kenya siyo tu yatahamasisha nchi nzima ya Sudan Kusini kwa uchaguzi mkuu ujao bali pia yataweka msingi wa amani ya kudumu nchini humo kwa kushirikisha makundi yote ya upinzani yaliyosalia.

Kuol ameliambia shirika la habari la China, Xinhua kuwa serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa imeona uwezekano wa kuleta kila mtu kwenye bodi kabla ya kuweza kuzungumza juu ya uchaguzi.

Sudan Kusini inatazamiwa kufanya uchaguzi wake mkuu mwezi Desemba, kwani kipindi cha mpito kilichoongezwa Agosti 2022 kitakamilika Februari 2025. Kuol amesema makubaliano ya amani ya Nairobi yataunganishwa na Makubaliano Yaliyofikiwa tena Mwaka 2018 kuhusu Usuluhishi wa Migogoro nchini Sudan Kusini, ambayo yaliratibiwa na kusimamiwa na Mamlaka ya Kiserikali kwa Maendeleo ya nchi za Afrika Mashariki (IGAD) ili kumaliza mgogoro wa miaka mingi tangu Desemba 2013.

Habari zaidi zinazonukuu Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) zinasema kuwa, watu zaidi ya milioni 7 kati ya watu milioni 11 wanaokadiriwa wa Sudan Kusini huenda wakakumbwa na kiwango kikubwa cha uhaba wa chakula hadi Julai.

OCHA imesema ghasia kati ya jamii, mgogoro wa kiuchumi na majanga yanayosababishwa na hali ya hewa yanatishia angalau watu 79,000 wanaokabiliwa na hatari kubwa ya janga la njaa.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha