Wataalamu wakutana nchini Kenya ili kuongeza ufikiaji wa kidijitali barani Afrika

(CRI Online) Mei 15, 2024

Wataalamu wameanza mkutano wa siku tatu mjini Nairobi, Kenya, ili kuhimiza upatikanaji wa huduma za kidijitali na teknolojia wezeshi kwa watu wanaoishi na ulemavu katika bara zima la Afrika.

Mkutano huo wa 5 wa Umoja wa Afrika wa 2024 unaofanyika chini ya kaulimbiu "Kuvunja Vikwazo: Kuboresha Upatikanaji wa Kidijitali kwa Mustakabali Jumuishi wa Watu wenye Ulemavu Barani Afrika", unawaleta pamoja washiriki zaidi ya 300, wakiwemo wataalamu, wavumbuzi, wajasiriamali na maafisa wa serikali kutoka kote barani Afrika ili kubadilishana maarifa juu ya namna ya kuondokana na vikwazo vilivyopo vya ujumuishaji wa kidijitali.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, mjumbe maalum wa Kenya katika masuala ya teknolojia, Phillip Thigo, amesema wakati zama hizi zinashuhudia maendeleo makubwa zaidi ya kiteknolojia, Afrika pia inashuhudia kuongezeka kwa pengo la ukosefu wa usawa katika upatikanaji wa teknolojia, hasa miongoni mwa watu wanaoishi na ulemavu barani Afrika.

Ameongeza kuwa teknolojia zinazoibukia kama vile blockchain zinaweza kuwajumuisha kifedha watu wenye ulemavu kwa kupanua ufikiaji wa huduma za benki na mikopo ambazo hazikuweza kupatikana hapo awali.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha