Kiongozi wa Kenya atafuta msaada wa kijeshi ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

(CRI Online) Mei 16, 2024

Rais wa Kenya William Ruto Jumatano ametoa wito kwa jeshi la nchi hiyo kuisaidia serikali kuimarisha juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza kwenye gwaride la kufunga mafunzo kwa maafisa wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) katika Chuo cha Mafunzo ya Makuruta huko Eldoret, Ruto amesema mabadiliko ya tabianchi ni tishio kubwa kwa maendeleo na ustawi wa nchi.

Ameeleza kuwa wakati wanalinda taifa lao dhidi ya vitisho vya usalama vinavyoibuka, mabadiliko ya tabianchi pia yatakuwa kitisho kikubwa, na kuongeza kuwa ndiyo maana lazima wahamasishe jeshi kutoa suluhisho kwa masuala yanayoibuka.

Kiongozi huyo wa Kenya amesema wanajeshi wanapaswa kuongoza kwa kutoa mbinu, wakishirikiana na Wizara ya Mazingira, ili kufikia lengo la upandaji miti bilioni 15 ifikapo 2032.

Wakati huohuo Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Ukame ya Kenya (NDMA) imesema mvua kubwa zimesababisha kaunti 23 katika ardhi kame na nusu kame nchini Kenya, ambazo kwa kawaida huathiriwa na ukame, kukumbwa na mafuriko makubwa. Mamlaka hiyo imebainisha kuwa mafuriko hayo makubwa yamedhoofisha usalama wa chakula katika maeneo kame.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha