Nchi za Mashariki ya Kati zatoa rambirambi kufuatia vifo vya rais na waziri wa mambo ya nje wa Iran

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 21, 2024
Nchi za Mashariki ya Kati zatoa rambirambi kufuatia vifo vya rais na waziri wa mambo ya nje wa Iran
Watu wakiomboleza watu waliokufa kwenye ajali ya helikopta karibu na Kaunti ya Varzaqan, mjini Tehran, Iran, Mei 20, 2024. (Xinhua/Shadati)

CAIRO - Viongozi wa nchi za Mashariki ya Kati wametuma salamu za rambirambi kwa Iran kufuatia vifo vya Rais Ebrahim Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian na maofisa wengine waliokuwa wameambatana naye kwenye ajali ya helikopta siku moja kabla.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Ahmed Aboul-Gheit amesema kupitia ujumbe wake kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X kwamba "Natoa rambirambi zangu kwa watu wa Iran kwa vifo vya Raisi, Amir-Abdollahian, na maofisa wengine kufuatia ajali mbaya ya ndege."

Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba Jasem Mohamed Albudaiwi ametoa rambirambi, na kusisitiza kuwa baraza hilo litashikamana na serikali na watu wa Iran katika nyakati ngumu, limeripoti Shirika rasmi la Habari la Saudi (SPA).

Mfalme wa Saudi Arabia Salman bin Abdulaziz Al Saud na Mwana Mfalme ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman Al Saud wametuma salamu za rambirambi kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran Mohammad Mokhber kutokana na vifo vya Raisi na maofisa wengine waliokuwa wameambatana nao, imesema taarifa iliyotolewa na SPA.

Ofisi ya rais wa Uturuki imetoa taarifa ikisema, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amemwambia Mokhber kwenye simu siku ya Jumatatu kwamba, Uturuki "inasimama na Iran katika siku hizi zenye uchungu" na "kuwa na masikitiko pamoja na watu wa Iran".

Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi ametoa salamu za rambirambi kwa watu wa Iran, akielezea mshikamano wa Misri na viongozi na watu wa Iran katika kipindi hiki cha msiba, Ikulu ya Misri imesema katika taarifa yake.

Aidha, Mfalme Abdullah II wa Jordan, Rais Abdul Latif Rashid wa Iraq, Rais wa Tunisia, Wizara ya Mambo ya Nje ya Libya pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Wahamiaji ya Lebanon na Mwenyekiti wa Baraza la Mamlaka ya Mpito la Sudan Abdel Fattah Al-Burhan pia wametoa salamu za rambirambi kwa serikali na watu wa Iran.

Ajali hiyo ilitokea Jumapili katika Kaunti ya Varzaqan ya Iran wakati Raisi, pamoja na timu yake wakiwa kwenye helikopta tatu, walikuwa wakitoka katika Kaunti ya Khoda Afarin, ambako alihudhuria uzinduzi wa bwawa la kuhifadhia maji na mwenzake wa Azerbaijan Ilham Aliyev mapema katika siku hiyo, kuelekea mji mkuu wa Jimbo la Tabriz kwa ajili ya uzinduzi wa mradi wa petrokemikali.

Maofisa wengine walioko kwenye helikopta iliyokuwa imembeba Raisi, akiwemo Gavana wa Azerbaijan Mashariki Malek Rahmati, Mwakilishi wa Kiongozi Mkuu wa Iran Ali Khamenei katika Azabajani Mashariki Mohammad Ali Ale-Hashem, mlinzi wa Raisi, pamoja na wafanyakazi wa ndege, pia wamepoteza maisha.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha