

Lugha Nyingine
Mji wa Shanghai watoa kadi za kulipia kabla ili kurahisisha wasafiri kutoka nchi za nje
Watalii wanaonekana kwenye picha wakielekea kwenye Jumba la Makumbusho ya Shanghai, Mashariki mwa China, tarehe 22 Mei, 2024. (Xinhua/Chen Aiping)
SHANGHAI – Mji wa Shanghai ulioko Mashariki mwa China umetoa Kadi ya Shanghai, ambayo ni kadi ya matumizi mbalimbali kwa ajili ya wasafiri, ili kuwezesha malipo rahisi kwa wasafiri wanaoingia mjini humo na wageni wengine ambao hawapendi kufanya malipo kwa njia ya simu.
Ikiwa na salio la juu la yuan zaidi ya 1,000 (kama dola 140 za Kimarekani), kadi ya Shanghai inaweza kutumika katika sehemu mbalimbali kama vile usafiri wa umma, maeneo ya kitamaduni na utalii, na maduka mengi, kwa mujibu wa Kampuni ya Kadi za Utalii ya Shanghai, ambayo inatoa kadi hizo.
Kadi hiyo inaweza kununuliwa na kuingizwa salio katika viwanja vya ndege vya Hongqiao na Pudong, na stesheni kubwa za sabwei kama vile Stesheni ya People's Square. Kadi hiyo inaweza kutumika katika mabasi, sabwei, teksi, feri, na vivutio vya utalii kama vile Mnara wa Shanghai wa Oriental Pearl, Jumba la Makumbusho ya Shanghai na Bustani ya Wanyamapori ya Shanghai, kampuni hiyo imesema.
Wenye kadi hiyo wanaweza kurejeshewa salio lililobaki wanapoondoka katika mji huo.
Wanaweza pia kutumia kadi hiyo kwa usafiri wa umma katika miji mingine mingi, ikiwa ni pamoja na Beijing, Guangzhou, Xi'an, Qingdao, Chengdu, Sanya na Xiamen, kampuni hiyo imesema.
Serikali ya China imechukua hatua kadhaa ili kurahisisha utalii kwa wageni wanaoingia nchini humo, kwani wageni ambao kimsingi wanategemea kadi za benki na pesa taslimu huenda watapata vizuizi na changamoto kufanya malipo yasiyohitaji pesa taslimu au kadi, ambayo kwa sasa ndiyo njia kuu ya malipo nchini China.
Shanghai ilipokea watalii milioni 1.27 walioingia kutoka nje katika robo ya kwanza ya mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la asilimia 250 mwaka hadi mwaka, na inatarajiwa kupokea watalii wapatao milioni 5 kwa mwaka mzima, kwa mujibu wa Idara ya Utamaduni na Utalii ya Shanghai.
Aiskrimu, kadi ya kulipia ya Pasi Shanghai na risiti ya manunuzi vikionekana pichani kwenye Jumba la Makumbusho ya Shanghai, Mashariki mwa China, Mei 22, 2024. (Xinhua/Chen Aiping)
Karani akiandaa malipo kwa kutumia kadi ya kulipia ya Pasi Shanghai kwenye duka la zawadi la Jumba la Makumbusho ya Shanghai, Mashariki mwa China, Mei 22, 2024. (Xinhua/Chen Aiping)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma