China na Nchi za Kiarabu kupaza sauti ya pamoja juu ya suala la Palestina

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 28, 2024

BEIJING - Deng Li, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumatatu kwamba, China na Nchi za Kiarabu zitapaza sauti ya pamoja kuhusu suala la Palestina kwenye Mkutano wa 10 wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Nchi za Kiarabu utakaofanyika Mei 30 mjini Beijing.

Deng amesema mkutano huo utaweka mkazo katika majadiliano ya kina na kujadili hatua halisi za utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa na wakuu wa nchi hizo, kupanua ushirikiano kati ya China na Nchi za Kiarabu katika sekta mbalimbali, na kuharakisha ujenzi wa jumuiya ya China na Nchi za Kiarabu yenye mustakabali wa pamoja.

Deng amedokeza kuwa, Mkutano huo unapanga kupitisha nyaraka mfululizo kuhusu matokeo ya mkutano, kuimarisha zaidi makubaliano kati ya China na Nchi za Kiarabu, kupanga ushirikiano wa kipindi kijacho, na kupaza sauti ya pamoja za China na Nchi za Kiarabu kuhusu suala la Palestina.

Deng amesema kuwa Rais Xi Jinping wa China atahudhuria hafla ya ufunguzi wa mkutano huo Mei 30 pamoja na Mfalme wa Bahrain Hamad bin Isa Al Khalifa, Rais wa Misri Abdel Fattah El-Sisi, Rais wa Tunisia Kais Saied, na Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan -- ambao wote watafanya ziara za kiserikali nchini China kuanzia leo Mei 28 hadi Juni 1.

Deng ameongeza kuwa, Rais Xi pia atatoa hotuba kuu katika hafla hiyo ya ufunguzi wa mkutano, na hayo yote yameonesha vya kutosha matarajio ya pamoja ya kufanya mshikamano na ushirikiano, na kusukuma uhusiano kati ya nchi za kiarabu kwenye ngazi mpya.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha