Trump akutwa na hatia katika makosa yote kwenye kesi ya kutoa mlungula

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 31, 2024

Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump (Kulia, Mbele) akiwa ameketi kwenye mahakama wakati wa kesi yake ya ulaghai wa kiraia katika Mahakama Kuu ya Jimbo la New York Marekani, Oktoba 18, 2023. (Jeenah Moon/ Xinhua)

Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump (Kulia, Mbele) akiwa ameketi kwenye mahakama wakati wa kesi yake ya ulaghai wa kiraia katika Mahakama Kuu ya Jimbo la New York Marekani, Oktoba 18, 2023. (Jeenah Moon/ Xinhua)

NEW YORK - Baraza la majaji mjini New York siku ya Alhamisi limetoa hukumu kuhusu Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump na hatia kwa mashtaka yote ya kesi ya kutoa mlungula, hukumu hiyo imesema Trump amekutwa na hatia kwenye makosa yote 34 ya kughushi rekodi za kibiashara kwa nia ya kuficha malipo ya dola za Kimarekani 130,000 ya kunyamazisha kashfa dhidi yake kwa nyota wa filamu za watu wazima Stormy Daniels Mwaka 2016, muda mfupi kabla ya uchaguzi wa rais.

Trump amekuwa rais wa kwanza wa zamani katika historia ya Marekani kukutwa na hatia ya uhalifu.

Baraza hilo la majaji 12 limefikia uamuzi huo siku ya Alhamisi alasiri baada ya usomaji na uchambuzi wa hoja za pande zote za mshtaki na mshitakiwa kuanza siku moja iliyopita.

Jaji Juan Merchan amekataa ombi la kuachiliwa huru kwa Trump na amepanga kusikilizwa kwa hukumu hiyo Julai 11.

Trump, ambaye anatarajiwa sana kukata rufaa baada ya hukumu hiyo kutolewa, amesema kesi hiyo dhidi yake ilikuwa "ya udanganyifu" na "aibu."

Trump na Wakili wa Wilaya ya Manhattan Alvin Bragg walitoka nje ya mahakama muda mfupi baada ya hukumu kusomwa na kuthibitishwa na majaji.

Kesi hiyo ilianza Aprili 15.

Akiwa ni rais wa kwanza wa zamani wa Marekani kushtakiwa katika kesi ya jinai na mgombea mteule wa urais anayetarajiwa wa chama cha Republican katika uchaguzi mkuu wa Mwaka 2024, Trump pia anakabiliwa na mashtaka mengine matatu ya jinai.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha