

Lugha Nyingine
Chama Tawala cha ANC cha Afrika Kusini chapata viti 159 katika Bunge la Taifa
(Picha inatoka photo.thepaper.cn)
JOHANNESBURG - Chama tawala cha Afrika Kusini, African National Congress (ANC) kimepata viti 159 kati ya 400 katika Bunge la Taifa la Afrika Kusini kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2024, Tume Huru ya Uchaguzi (IEC) imetangaza rasmi jana Jumapili jioni huku chama kikuu cha upinzani, Democratic Alliance (DA), kikishika nafasi ya pili kwa viti 87, kikifuatiwa na Chama cha Umkhonto WeSizwe (MK) chenye viti 58 na kile cha Economic Freedom Fighters (EFF) kilichopata viti 39.
Kwa mujibu wa matokeo rasmi ya uchaguzi yaliyotolewa na IEC katika Kituo cha Uchakataji Matokeo (ROC) huko Midrand, Johannesburg, Waafrika Kusini zaidi ya milioni 27 wameshiriki kwenye uchaguzi huo wa kitaifa na wa majimbo wa Mwaka 2024 uliofanyika Mei 29 ili kuchagua Bunge jipya la Taifa na mabaraza ya majimbo.
Hatimaye, hakuna chama kilichopata wingi wa viti kuweza kupata udhibiti wa Bunge la Taifa. ANC imepata viti chini ya 200 ilichohitaji ili kudumisha utawala wake usiopingwa uliodumu kwa miaka 30 katika baraza la chini la bunge.
Akitangaza matokeo hayo ya mwisho, Mwenyekiti wa IEC Mosotho Moepya ameutangaza uchaguzi mkuu wa 2024 kuwa wa "huru na wa haki."
Akiuita "uchaguzi ngumu zaidi na wenye ushindani mkubwa" tangu mwisho wa ubaguzi wa rangi mwaka 1994, Moepya amesema uchaguzi wa mwaka huu haukukosa changamoto zake, kwani majaribio ya kudhoofisha uaminifu wa IEC yamefanywa.
Katika hotuba yake baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo ya uchaguzi, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema "yanawakilisha ushindi kwa demokrasia yetu, kwa utaratibu wetu wa kikatiba na kwa watu wote wa Afrika Kusini."
Kufuatia kutangazwa rasmi kwa matokeo hayo ya uchaguzi siku ya Jumapili, Bunge jipya lililochaguliwa litakuwa na siku 14 kufanya mkutano wake wa kwanza, ambapo wajumbe watamchagua rais wa Afrika Kusini wa kipindi cha miaka mitano ijayo kwa wingi wa kura.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma