

Lugha Nyingine
China yapinga vikali vizuizi vya viza vya Marekani dhidi ya maofisa wa China
BEIJING - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Mao Ning kwenye mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumatatu amesema kuwa China inapinga vikali hatua ya Marekani kuingilia mambo ya ndani ya China baada ya Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kutangaza vizuizi vipya vya viza dhidi ya maofisa wa Serikali Kuu ya China na serikali ya Mkoa wa Utawala Maalum wa Hong Kong (HKSAR) katika taarifa iliyotolewa wiki iliyopita kuhusu hukumu iliyotolewa na mahakama ya Hong Kong juu ya baadhi ya waliohusika katika kesi ya kula njama ya kufanya uasi.
Amesema kwamba Marekani imelaumu kwa makusudi kanuni ya "nchi moja, mifumo miwili," imepaka matope Sheria ya Kulinda Usalama wa Nchi katika Hong Kong, imetoa maoni bila kuwajibika juu ya demokrasia na uhuru huko Hong Kong, na kutaka kuingilia masuala ya mahakama ya Hong Kong na kutumia vibaya vizuizi vya visa.
"Hatua hizo zinaingilia waziwazi mambo ya ndani ya China, zinakiuka sheria za kimataifa na kanuni za msingi zinazosimamia uhusiano wa kimataifa. China inasikitishwa na kupinga vikali," amesema msemaji huyo.
Ameongeza kuwa kile kinachoitwa "uchaguzi wa msingi" ulioandaliwa na wale waliohusika katika kesi hiyo ambao wanaipinga China na kutaka kuvuruga utulivu wa Hong Kong ni sawa na kwenda kinyume kwa kiasi kikubwa na utaratibu wa kikatiba wa Hong Kong na kuhatarisha usalama wa nchi .
"Kati ya washtakiwa waliohusika katika kesi hiyo, 31 tayari wamekiri makosa," Msemaji huyo amesema, huku akibainisha kuwa ni jambo la busara na halali kwa vyombo vya kusimamia utekelezaji wa sheria na mahakama katika Hong Kong kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, na kuadhibu vitendo vyote vinavyohatarisha usalama wa nchi, na kwamba inaungwa mkono kithabiti na Serikali Kuu ya China.
Amesisitiza kuwa mambo ya Hong Kong ni mambo ya ndani ya China ambayo hayahitaji uingiliaji wowote wa nje.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma