Putin asema Uhusiano wa Russia na China uliopo kwenye msingi wa maslahi ya pamoja unasaidia utulivu wa Dunia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 06, 2024

ST. PETERSBURG - Rais wa Russia Vladimir Putin siku ya Jumatano alipokuwa akijibu swali lililotolewa na Shirika la Habari la China, Xinhua, kuhusu uhusiano kati ya Russia na China, kwenye mkutano na wakuu wa mashirika makubwa ya habari ya kimataifa, amesema kwamba maendeleo ya uhusiano kati ya Russia na China kwenye msingi wa maslahi ya kina ya pamoja unasaidia utulivu wa Dunia.

"Kuendeleza uhusiano kati ya Russia na China siyo vitendo vya muda mfupi, uhusiano huo unaendelea kwenye msingi wa maslahi ya kina ya pamoja, na uhusiano wa nchi hizo mbili unategemea kufanya maamuzi kwa busara na juhudi zilizofanywa kwa pamoja katika siku nyingi zilizopita," Rais Putin amesema.

Rais Putin amebainisha kuwa China imekuwa mshirika mkuu wa Russia wa kiuchumi na kibiashara kwa miaka 15 iliyopita. Biashara kati ya nchi hizo mbili imezidi matarajio, na kufikia thamani ya dola za kimarekani bilioni 240 mwaka jana kwa mujibu wa takwimu za China. Wakati huo huo, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Russia na China unazidi kuwa wa aina mbalimbali, pamoja na sekta ya nishati, na pande hizo mbili pia zina matarajio mapana ya ushirikiano katika sekta za teknolojia ya hali ya juu kama vile utengenezaji wa ndege na akili mnemba.

Amesisitiza kuwa ushirikiano wa pande mbili ni zaidi ya sekta za uchumi na biashara, mambo ya kijeshi na teknolojia pamoja na majukwaa ya kimataifa. Ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika majukwaa ya kimataifa umekuwa jambo muhimu katika kudumisha utulivu wa Dunia.

Mwaka huu ni Mwaka wa Utamaduni wa Russia na China, Rais Putin amesema, huku akiongeza kuwa mawasiliano ya kitamaduni yanaweka msingi na kujenga mazingira mazuri ya maendeleo ya uhusiano wa pande mbili na ushirikiano katika sekta mbalimbali, jambo ambalo ni muhimu sawa na mambo ya sekta nyingine.

Akizungumzia mafanikio ya maendeleo ya China, Rais Putin amesema chini ya uongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), China imepata mafanikio katika sekta mbalimbali za maendeleo, hali ambayo Russia inafurahishwa nayo.

Mkutano huo wa vyombo vya habari uliandaliwa na shirika la habari la Russia, TASS pembezoni mwa Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg 2024. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha