Mahakama ya rufaa yasimamisha kesi ya Trump ya uchaguzi wa Mwaka 2020 katika Jimbo la Georgia la Marekani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 06, 2024

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump (Mbele) akiongea na waandishi wa habari nje ya chumba cha mahakama wakati wa kesi yake ya ulaghai wa kiraia katika Mahakama Kuu ya Jimbo la New York mjini New York, Marekani, Oktoba 18, 2023. (Picha na Michael Nagle/Xinhua)

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump (Mbele) akiongea na waandishi wa habari nje ya chumba cha mahakama wakati wa kesi yake ya ulaghai wa kiraia katika Mahakama Kuu ya Jimbo la New York mjini New York, Marekani, Oktoba 18, 2023. (Picha na Michael Nagle/Xinhua)

WASHINGTON - Mahakama ya rufaa ya Jimbo la Georgia nchini Marekani siku ya Jumatano imesimamisha mchakato wa kesi inayomhusu Rais wa zamani wa nchi hiyo Donald Trump ya kupindua matokeo ya uchaguzi mkuu wa Mwaka 2020 kwa lengo la kutathmini upya rufaa hizo.

Trump na wengine 18 walishtakiwa mwezi Agosti mwaka jana kwa madai ya kupindua matokeo ya uchaguzi wa urais wa Mwaka 2020 katika jimbo hilo la kusini mashariki mwa Marekani. Trump amekana mashtaka na kukosoa kesi hiyo dhidi yake akiielezea kuwa ni sehemu ya jaribio la kisiasa la kumzuia kutwaa tena Ikulu ya White House.

Amri hiyo kutoka Mahakama ya Rufaa ya Georgia imetolewa baada ya mahakama hiyo mapema wiki hii kupanga tarehe ya kusikilizwa kwa rufaa hiyo mwezi Oktoba. Trump na washtakiwa wenzake kadhaa katika kesi hiyo wamedai kuwa uhusiano wa Mwanasheria wa Wilaya ya Kaunti ya Fulton Fani Willis na mwendesha mashtaka maalum wa wakati huo Nathan Wade ulisababisha mgongano wa kimaslahi.

Trump na baadhi ya washitakiwa wenzake katika kesi hiyo ya ulaghai wamekuwa wakijaribu kumfanya Willis aondolewe kwa kukosa vigezo kwenye kesi hiyo kwa sababu ya uhusiano wa kimapenzi aliokuwa nao na Wade, mwendesha mashtaka maalum aliyemwajiri kusaidia kushughulikia kesi hiyo, limeripoti Shirika la Utangazaji la CNN, huku likiongeza kuwa washtakiwa hao wamedai kuwa Willis alinufaika kifedha kutokana na uhusiano na Wade, ambaye mawakili wa upande wa utetezi wanasema aligharamikia likizo kadhaa kwa wawili hao.

CNN imedokeza kuwa amri hiyo mpya ni dalili mpya kwamba kesi hiyo katika ngazi ya jimbo la Georgia ya kupindua matokeo ya uchaguzi haitatokea kabla ya uchaguzi wa urais wa Mwaka 2024.

Trump, ambaye ni mgombea mteule mtarajiwa wa kiti cha urais wa Chama cha Republican kwenye uchaguzi mkuu wa Mwaka 2024, amefunguliwa mashtaka katika kesi nne za uhalifu - mbili na Wizara ya Sheria ya Marekani, na mbili na waendesha mashtaka wa serikali za majimbo ya New York na Georgia, mtawalia. Kesi ya Georgia ni kesi ya nne kufunguliwa dhidi ya Trump.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha