Karibu watu 134,000 waathirika na uhaba wa chakula kusini mwa Msumbiji

(CRI Online) Juni 11, 2024

Watu 133,974 wanakabiliwa na uhaba wa chakula katika mkoa wa Gaza, kusini mwa Msumbiji kutokana na mavuno hafifu ya mazao ya kilimo yaliyosababishwa na mvua kidogo zilizonyesha katika msimu wa kilimo wa mwaka 2023/2024.

Takwimu hizo zimetolewa jumatatu na msemaji wa Mkutano wa Kawaida wa 10 wa Baraza la Huduma za Wawakilishi wa mkoa wa Gaza, Alberto Matusse. Amesema pamoja na kwamba mvua zilinyesha katika miezi ya Machi na April mwaka huu, kiasi cha maji hakikutosheleza kuboresha mazao.

Ameongeza kuwa, wilaya zilizoathirika zaidi kutokana na uhaba wa mvua katika mkoa huo ni Guija, Chigubo, Mabalane, Mapai, Chicualacuala na Massangena.

Gaza ni mkoa unaojulikana kwa kilimo nchini Msumbiji na ni maarufu kwa uzalishaji wa nafaka na mchele.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha