Botswana yaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Watoto Kucheza kwa mara ya kwanza kabisa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 12, 2024

Alexandra Illmer, Naibu Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watoto Kucheza huko Gaborone, Botswana, Juni 11, 2024. (Picha na Tshekiso Tebalo/Xinhua)

Alexandra Illmer, Naibu Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watoto Kucheza huko Gaborone, Botswana, Juni 11, 2024. (Picha na Tshekiso Tebalo/Xinhua)

GABORONE - Botswana imeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Watoto Kucheza kwa mara ya kwanza kabisa siku ya Jumanne kwa kuandaa sherehe ya kufurahisha iliyoshirikiwa na watoto. Tarehe 11 Juni ya kila mwaka iliteuliwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Watoto Kucheza na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kuendeleza na kulinda haki ya watoto ya kucheza.

Shughuli hiyo ya Jumanne, iliyohudhuriwa na walimu, wahudumu wa afya na wadau, ilihusisha kucheza soka, kucheza muziki na kuimba. Baadhi ya watoto walicheza na wanasesere na kuchora picha. Hafla hiyo iliandaliwa na shirika la hisani la Learn to Play, kwa ushirikiano na Halmashauri ya Jiji la Gaborone na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).

Shughuli hizo zimelenga kuongeza furaha na kujifunza kwa watoto, na vile vile kukutanisha pamoja wadau, washawishi wa jamii, na watunga sera ili kusaidia kuhakikisha mipango ya maendeleo ya mapema ya watoto ambayo ni fanisi, jumuishi na inayofikika na watu wengi, amesema Priyanka Handa Ram, mwanzilishi mwenza na mtendaji mkuu wa shirika hilo la Learn to Play huko Gaborone, mji mkuu wa Botswana.

Learn to Play ni shirika la kutoa misaada lililoanzishwa Mwaka 2017 ili kuunda mzunguko endelevu wa mageuzi kwa kizazi kijacho cha watoto wa Botswana.

Kwenye hafla hiyo hiyo, Alexandra Illmer, naibu mwakilishi wa UNICEF nchini humo, amesema siku hiyo ni hatua muhimu katika juhudi zao za pamoja za kulinda, kuendeleza na kutanguliza kucheza, ili kuhakikisha kwamba watu wote, hasa watoto, wanaweza kupata manufaa yake makubwa na kustawi katika uwezo wao kikamilifu.

"Kucheza siyo tu kupitisha muda; ni msingi ambao ukuaji wa mapema wa afya ya utotoni hujengwa juu yake. Kupitia kucheza, watoto hujenga ujuzi muhimu wa utambuzi, wa kimwili, wa ubunifu, wa kijamii na wa kihisia unaohitajika ili kujiongoza na kustawi katika ulimwengu wetu unaobadilika haraka," amesema.

Watoto wakishiriki kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watoto Kucheza huko Gaborone, Botswana, Juni 11, 2024. (Picha na Tshekiso Tebalo/Xinhua)

Watoto wakishiriki kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watoto Kucheza huko Gaborone, Botswana, Juni 11, 2024. (Picha na Tshekiso Tebalo/Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha