

Lugha Nyingine
Waziri wa Mambo ya Nje wa China akutana na mwenzake wa Afrika Kusini
NIZHNY NOVGOROD - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amekutana na mwenzake wa Afrika Kusini Naledi Pandor siku ya Jumatatu katika Mji wa Nizhny Novgorod nchini Russia ambapo ameipongeza Afrika Kusini kwa uchaguzi mkuu wa amani na kukipongeza chama cha African National Congress (ANC) kwamba kitaendelea kuonesha umuhimu wake wa uongozi katika siasa za Afrika Kusini kikiwa ni chama kikubwa zaidi.
Wang, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), ameeleza imani yake kwamba ANC itaendelea kutimiza matarajio yake ya awali, kushikilia kithabiti imani yake, na kuendelea kuwaongoza watu wa Afrika Kusini kupata mafanikio makubwa zaidi katika kujenga nchi yenye muungano, utulivu na ustawi.
Wang amebainisha kuwa China na Afrika Kusini ni washirika wa kimkakati wa pande zote na uhusiano wa pande mbili unastawi chini ya mwongozo wa kimkakati wa wakuu wa nchi hizo mbili, ukidhihirisha "zama ya dhahabu."
Mwaka jana, Rais Xi Jinping wa China alifanya ziara ya kiserikali nchini Afrika Kusini, kuhudhuria kwenye Mkutano wa wakuu wa nchi za BRICS, kufikia makubaliano muhimu na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, na kuanzisha nyakati mpya za kujenga jumuiya ya ngazi ya juu ya China na Afrika Kusini yenye mustakabali wa pamoja, amesema Wang, huku akiongeza kuwa upanuzi wa kihistoria wa mfumo wa BRICS uliotangazwa nchini Afrika Kusini umechochea zaidi mshikamano kati ya Nchi za Kusini.
Wang amesema kuwa pande hizo mbili zinapaswa kuimarisha mabadilishano ya ngazi ya juu, kuongeza hali ya kuaminiana kisiasa, kupanga mawasiliano ya kitaasisi katika kipindi kijacho, na kuendelea kuungana mkono kithabiti katika masuala yanayohusu masilahi ya msingi ya kila mmoja.
Kwa upande wake, Pandor ameishukuru China kwa uungaji mkono wake kwa Afrika Kusini katika kufanikisha kuandaa mkutano wa wakuu wa nchi za BRICS, akisema kuwa nchi yake imepata heshima kubwa kupokea ziara ya Rais Xi mwaka jana.
Amesema Afrika Kusini na China zinadumisha uhusiano thabiti wa pande mbili, huku kampuni za China zikiendelea kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Afrika Kusini, mawasiliano kati ya pande mbili katika mambo ya utamaduni yakiendelea kuwa ya karibu, na ushirikiano katika sekta mbalimbali unaendelea vizuri.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma