

Lugha Nyingine
Waziri Mkuu wa China Li Qiang awasili New Zealand kwa ziara rasmi
WELLINGTON - Waziri Mkuu wa China Li Qiang amewasili mjini Wellington leo Alhamisi kuanza ziara rasmi nchini New Zealand, ikiwa ni kituo cha kwanza cha ziara yake ya nchi tatu kuanzia Juni 13 hadi 20 ambapo amesema anatarajia kuwa na mazungumzo ya kina na viongozi wa New Zealand na watu wa makundi mbalimbali kuhusu uhusiano kati ya China na New Zealand na masuala yanayohusu maslahi ya pamoja, kuzidisha zaidi mawasiliano na ushirikiano katika sekta mbalimbali, na kuboresha uhusiano wa wenzi wa ushirikiano wa kimkakati wa pande zote kati ya China na New Zealand.
Mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 10 tangu ziara ya Rais Xi Jinping wa China nchini New Zealand, pamoja na kuanzishwa kwa uhusiano wa wenzi wa ushirikiano wa kimkakati wa pande zote kati ya China na New Zealand, Li amesema, huku akibainisha kuwa ziara yake nchini New Zealand inalenga kuendeleza urafiki wa jadi, kuongeza ushirikiano wa kunufaishana, na kuhimiza maendeleo kwa pamoja.
Ingawa China na New Zealand zimetenganishwa na bahari kubwa, mawasiliano yao ya kirafiki yamekuwa na historia ndefu, na zina maelewano ya kina na uhusiano wa karibu kwa kila upande, Li amesema.
Li ameongeza kuwa, kwa zaidi ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia chini ya mwongozo wa kimkakati wa viongozi wa nchi zote mbili, uhusiano kati ya China na New Zealand umekuwa safu ya mbele katika uhusiano wa China na nchi zilizoendelea.
Li ameeleza imani yake kwamba kwa juhudi za pamoja, uhusiano kati ya China na New Zealand hakika utaingia katika kipindi cha mustakabali mzuri zaidi, na kuleta manufaa zaidi kwa watu wa nchi zote mbili na kuchangia zaidi amani, utulivu, maendeleo na ustawi wa Dunia.
Wakati wa ziara yake nchini humo, Li atafanya mazungumzo ya kina na Gavana Mkuu Cindy Kiro, Waziri Mkuu Christopher Luxon na maofisa wengine kuhusu uhusiano wa China na New Zealand pamoja na masuala ya kimataifa na ya kikanda ambayo yanafuatiliwa kwa pamoja.
Li pia atafanya ziara rasmi nchini Australia na Malaysia, na yeye na Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese wataendesha pamoja Mkutano wa tisa wa Mwaka wa Viongozi wa China na Australia.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma