

Lugha Nyingine
Chama cha ANC cha Afrika Kusini chasema kinatazamia serikali ya umoja wa kitaifa
Katibu Mkuu wa African National Congress (ANC) Fikile Mbalula (Kulia) akitoa maelezo kwa wanahabari baada ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya ANC mjini Cape Town, Afrika Kusini, Juni 13, 2024. (Picha na Xabiso Mkhabela/Xinhua)
CAPE TOWN - Chama tawala cha Afrika Kusini, African National Congress (ANC) kinatazamia kuanzishwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, amesema Katibu Mkuu wa chama hicho Fikile Mbalula siku ya Alhamisi, siku moja kabla ya kikao cha kwanza cha Bunge la Taifa, ambalo ni baraza la chini la bunge, leo Ijumaa ambacho kitamchagua rais wa Afrika Kusini kwa miaka mitano ijayo.
"ANC inatazamia kuanza kwa bunge la saba la kidemokrasia na kuanzishwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa," Mbalula ameuambia mkutano na waandishi wa habari baada ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya ANC uliofanyika Jumatano jioni huko Cape Town, Afrika Kusini.
Mbalula amesema timu ya majadiliano ya chama chake katika wiki iliyopita imefanya mazungumzo na majadiliano mengi na vyama vya siasa ambavyo vimepata viti bungeni, ikiwa ni pamoja na chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance, Inkatha Freedom Party na makundi mengine madogo madogo.
"Tumepata mafanikio juu ya makubaliano ya pamoja kwamba tunahitaji kufanya kazi kwa pamoja, iwe wengine wanavyoiita serikali hii ya umoja wa kitaifa au wanaoiita kitu kingine chochote kwa suala hilo," amebainisha. "Lakini tumekubaliana na vyama hivi vya siasa kwamba tunahitaji kuvuka katikati." Amesema Katibu Mkuu huyo wa ANC pia amesisitiza kuwa chama chake "hakitarudi nyuma juu ya dhana ya serikali ya umoja wa kitaifa, kwa sababu tunaamini kuwa serikali ya umoja wa kitaifa, kwetu, inawakilisha matokeo ya uchaguzi."
"Hatukupata viti vingi vya kutosha," Mbalula amesema. "Hatuko katika nafasi ya kutawala nchi hii peke yetu."
Kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Mei 29, ANC ilipata viti 159 kati ya 400 katika Bunge la Taifa, kwa mara ya kwanza kikishuka chini ya asilimia 50 inayohitajika kudumisha wingi wa wabunge wake usiopingwa wa baraza hilo la chini la Bunge katika kipindi cha miaka 30 iliyopita.
Katibu Mkuu wa African National Congress (ANC) Fikile Mbalula (Kulia) akitoa maelezo kwa wanahabari baada ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya ANC mjini Cape Town, Afrika Kusini, Juni 13, 2024. (Picha na Xabiso Mkhabela/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma