

Lugha Nyingine
Kampuni ya China yatumia vishikwambi vinavyotumia nishati ya jua kuongeza ujuzi wa ufundi kwa jamii za Kenya ambazo hazijaunganishwa kwenye gridi ya taifa
Wanawake wenyeji nchini Kenya wakishiriki kwenye somo la usukaji na ufungaji wa nywele linalotolewa kwa nji ya vishikwambi vinavyotumia nishati ya jua katika saluni ya muda huko Makueni, Kenya, Juni 6, 2024. (Picha na Lin Jing/Xinhua)
NAIROBI – Katika kaunti ya Makueni, kusini-mashariki mwa Kenya, shamba lenye ukubwa wa ekari kumi la Christine Musyoki linajitokeza wazi katikati ya majani mabichi yaliyosababishwa na mvua kubwa ya hivi karibuni.
Mama huyo wa watoto wanne ambaye ni mwalimu mtaaluma alikuwa akitembea shambani, akinyoosha kidole kuonesha mazao ya lettusi, vitunguu, nyasi za mifugo na mahindi ambayo yatavunwa hivi karibuni na kuuzwa kwenye masoko katika miji ya karibu.
Umahiri wa Musyoki katika kilimo cha biashara umechangiwa na mafunzo aliyopata kutoka kwenye kishikwambi kinachotumia nishati ya jua, kilichopewa jina la "Solar Media" kilichotolewa na kampuni ya Kuendesha Nishati ya Jua ya Shenzhen ya China kwa ushirikiano na shirika la hisani la nchini Kenya, Mama Layla Solar Lights.
Shukrani kwa masomo ya kilimo yaliyoingizwa awali kwenye kishikwambi hicho, Musyoki amepata maarifa na ujuzi wa kulima mboga, vitunguu na mikunde kwenye shamba lake, lililoko umbali wa kilomita 78 kusini-mashariki mwa Nairobi, mji mkuu wa Kenya.
"Tangu nianze kutumia Solar Media, lazima niseme mavuno ni mengi. Nimejifunza ujuzi mwingi kutoka kwenye solar media. Nimejifunza kuhusu kuweka nafasi kati ya mazao, ujuzi wa kunyunyiza, matumizi ya kemikali na dawa," Musyoki ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwenye mahojiano ya hivi karibuni katika shamba kwake.
Vikiwa vimeundwa ili kuwezesha jamii ambazo hazijaunganishwa kwenye gridi ya taifa ya umeme na zilizo maeneo ya pembezoni ya vijijini nchini Kenya kupitia kutoa masomo yaliyoandaliwa tayari juu ya ujuzi wa ufundi kama vile kilimo-biashara, ushonaji nguo na upambaji wa nywele, vishikwambi hivyo vinavyotumia nishati ya jua vilizinduliwa kwa mara ya kwanza Septemba 2022.
Familia zaidi ya 200 katika maeneo ya pembezoni ya vijijini katika nchi hiyo zimenufaika kutokana na utekelezaji wa mradi huo wa Solar Media, huku vishikwambi 25 na 81 vikiwa vimesambazwa katika awamu ya kwanza na ya pili mtawalia.
Vishikwambi takriban 200 vilivyounganishwa na nishati ya jua vilikuwa vikitarajiwa kusambazwa nchi nzima Novemba 2023 wakati wa utekelezaji wa awamu ya tatu ya mradi huo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo ya nishati ya jua ya Shenzhen.
Musyoki ni miongoni mwa wakulima wa vijijini nchini Kenya ambao kutumia vishikwambi hivyo kumewaletea mageuzi, vikiwapa taarifa rahisi kusomeka kuhusu kulima, kupanda, kupalilia, kuweka mbolea, na kumwagilia mimea yao.
Jane Triza Akinyi, mtaalamu wa kilimo katika shirika la hisani la Mama Layla, amesema vishikwambi hivyo vina nyenzo onyeshi na maandishi yaliyoingizwa awali ili kuelimisha wakulima juu ya aina mbalimbali za mazao, kuweka nafasi kati ya mazao, jinsi ya kushughulikia vifaa vya kilimo, na usimamizi baada ya kuvuna.
Tangu ilipoingia katika soko la Kenya miaka 15 iliyopita, Kampuni hiyo ya Nishati ya Jua ya Shenzhen imeimarisha upatikanaji wa umeme miongoni mwa jamii za vijijini zisizounganishwa kwenye gridi ya taifa, na kubadilisha maisha yao, amesema Li Xia, mwanzilishi wa kampuni hiyo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma