

Lugha Nyingine
Taarifa ya G7 kuhusu China imejaa kiburi, chuki: Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China
BEIJING - Taarifa iliyotolewa na G7 kwa mara nyingine tena imevumisha masuala yanayohusiana na China, na kukashifu nchi hiyo kwa madai yasiyo na msingi yanayokosa msingi wa ukweli wa mambo, misingi ya kisheria, na maadili, ambayo ni tabia iliyojaa kiburi, chuki na uongo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Lin Jian amesema Jumatatu.
Lin amesema hayo kwenye mkutano na wanahabari wakati akijibu Taarifa iliyotolewa na Viongozi wa G7, ambayo imetoa maoni ya kutowajibika kuhusu hali ya Mlango-Bahari wa Taiwan, pia kuhusu masuala yanayohusiana na Bahari ya Mashariki ya China, Bahari ya Kusini ya China, Hong Kong, Xinjiang na Xizang, na juu ya kile kinachoitwa "uzalishaji bidhaa kupita kiasi wa China."
G7 haiwakilishi Dunia, Lin amebainisha, huku akisema nchi hizo saba zinachangia asilimia 10 pekee ya watu wote duniani na sehemu yao katika uchumi wa Dunia imekuwa ikishuka mwaka baada ya mwaka. Ameongeza kuwa hata zikiunganishwa, zinachangia kidogo kuliko China kwenye ukuaji wa uchumi wa dunia, na thamani ya jumla ya uchumi wao katika suala la usawa wa uwezo wa manunuzi tayari umepitwa na nchi za BRICS.
Amesema kuwa G7 imepotoka kwa muda mrefu kutoka kwenye madhumuni yake ya awali ya kuratibu utulivu wa mazingira ya uchumi wa Dunia, na imezidi kuwa chombo cha kisiasa cha kuendeleza ubabe wa Marekani na nchi za Magharibi.
"Inaweka sheria na maamuzi yake juu ya madhumuni na kanuni za Katiba ya Umoja wa Mataifa na sheria ya kimataifa, na imepoteza uwezo wake wa kuwakilisha Dunia na uaminifu wake kati ya jumuiya ya kimataifa," ameongeza.
Kundi la G7 linachukua hatua dhidi ya mwelekeo wa Dunia wa maendeleo ya amani, Lin amebainisha, huku akisema kwamba wakati inadai kulinda amani ya Dunia, G7 inaendelea kuchora mstari katika tofauti za itikadi na maadili, na kuvumisha simulizi ya uongo ya "demokrasia dhidi ya udikteta," kuunda makundi na makabiliano ya kambi, kuchochea moto na kukwepa majukumu katika migogoro ya kikanda, kutuma meli na ndege za kijeshi katika eneo la Asia-Pasifiki ili kuleta hali ya wasiwasi, na kuipa Taiwan silaha ili kutishia amani na utulivu katika Mlango wa Bahari wa Taiwan.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma