

Lugha Nyingine
Jumuiya ya Afrika Mashariki yakutana nchini Kenya kujadili uanachama wa Somalia
NAIROBI - Wajumbe kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wameanza mkutano wa wiki moja siku ya Jumatatu mjini Nairobi, Kenya, ili kuandaa dira kabambe ya kuijumuisha Somalia kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katibu Mkuu wa EAC Veronica Mueni Nduva, ambaye alifungua rasmi mkutano huo, ameangazia muktadha wa kihistoria na umuhimu wa dira hiyo ya Somalia kujiunga na jumuiya hiyo.
Nduva amesema Somalia ilipata uanachama kamili wa EAC mwezi Machi baada ya kuweka rasmi hati yake ya kuridhia Mkataba wa Kujiunga kwa Katibu Mkuu wa EAC mjini Arusha, Tanzania.
"Mkutano wa leo unaashiria hatua muhimu katika safari hii, kuoanisha michakato ya kitaifa ya Somalia na mifumo ya kikanda ili kuhakikisha mchakato kamili wa kujiunga," amesema, katika taarifa iliyotolewa na Sekretarieti ya EAC.
Kujiunga kwa Somalia katika EAC kutaiwezesha nchi hiyo kunufaika na miradi ya miundombinu ya kikanda ya EAC, kama vile barabara, reli na mitandao ya nishati.
Nduva amesema dira hiyo itahusisha shughuli zitakazofanywa kwa pamoja na Somalia na vyombo na taasisi za EAC.
Ameongeza kuwa dira hiyo, ikishahitimishwa, itatumika kama zana ya kimkakati ya kuoanisha miradi na kuhamasisha rasilimali kwa ufanisi katika jumuiya hiyo ya kikanda.
"Miradi hii inalenga kuboresha muunganisho, kuimarisha miunganisho ya usafirishaji, na kuongeza biashara ya kikanda, na hatimaye kusaidia maendeleo ya kiuchumi na kujiunga kwa Somalia," Nduva amesema.
Abdusalam H. Omer, mjumbe maalum wa rais wa Somalia, ameeleza matumaini yake kuhusu juhudi za ushirikiano za washikadau wote katika kuunda dira ambayo itahakikisha Somalia kujiunga na jumuiya hiyo.
"Somalia inaendelea kuwa imara katika dhamira yake ya kutimiza malengo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuongeza umoja, ustawi na amani katika kanda nzima," amesema.
Somalia itachagua wabunge tisa katika Bunge la Afrika Mashariki na kumteua jaji wa Kitengo cha Kwanza cha Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki, ikiimarisha zaidi dhamira yake katika mchakato wa utandawazi wa kikanda.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma