

Lugha Nyingine
Cyril Ramaphosa aapishwa kuwa rais wa Afrika Kusini kwa muhula wa pili
Cyril Ramaphosa (Kulia) akila kiapo cha kuwa rais wa Afrika Kusini kwenye hafla ya kuapishwa kwake mjini Pretoria, Afrika Kusini, Juni 19, 2024. (Xinhua/Zhang Yudong)
JOHANNESBURG - Cyril Ramaphosa, kiongozi wa chama tawala cha Afrika Kusini cha African National Congress (ANC), amekula kiapo cha kuwa rais wa taifa hilo kwa miaka mitano ijayo siku ya Jumatano kwenye hafla iliyofanyika Pretoria, mji mkuu wa utawala wa nchi hiyo.
“Nikiwa rais wa nchi hiyo, nitashirikiana na kila mtu kushauriana na kufanya kazi na kila chama cha siasa na sekta ambayo inatoa mchango katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili nchi yetu tunapoelekea katika muongo mpya wa uhuru,” Ramaphosa amesema katika hotuba yake kwenye hafla hiyo.
Ramaphosa, mwenye umri wa miaka 71, alichaguliwa tena kuwa rais wa Afrika Kusini na Bunge la Kitaifa, baraza la chini la bunge la nchi hiyo, Juni 14, akipata kura 283. Mpinzani wake, Julius Malema kutoka chama cha Economic Freedom Fighters, alipata kura 44. Kwa mujibu wa Katiba ya Afrika Kusini, mara baada ya kuchaguliwa na Bunge, rais mteule lazima achukue madaraka ndani ya siku tano.
"Tutaalika vyama vyote, mashirika ya kiraia, wafanyakazi, wafanyabiashara na mashirika mengine kwenye mazungumzo ya kitaifa juu ya changamoto kuu zinazolikabili taifa. Tutatafuta, kama tulivyofanya katika nyakati muhimu sana katika historia yetu, kuunda makubaliano ya kijamii ili kutimiza matarajio ya Mpango wetu wa Maendeleo wa Taifa,” amesema Ramaphosa, huku akisisitiza umuhimu wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.
Kwenye uchaguzi mkuu wa Mei 29, chama cha ANC kilipata viti 159 kati ya 400 katika Bunge la Kitaifa, ikishuka chini ya asilimia 50 inayohitajika kudumisha wingi wa wabunge wake bungeni wa miaka 30 katika baraza la chini la bunge kwa mara ya kwanza.
Chama cha ANC siku ya Jumatatu kilitangaza kuwa jumla ya vyama vitano vya kisiasa vikiwemo ANC, Democratic Alliance, Inkatha Freedom Party, GOOD na Muungano wa Patriotic, vimetia saini rasmi taarifa ya nia ya kushiriki katika serikali ya umoja wa kitaifa.
Helikopta ikiruka juu ya hafla ya kuapishwa kwa Rais Cyril Ramaphosa mjini Pretoria, Afrika Kusini, Juni 19, 2024. (Xinhua/Zhang Yudong)
Cyril Ramaphosa (Kulia) akila kiapo cha kuwa rais wa Afrika Kusini kwenye hafla ya kuapishwa kwake mjini Pretoria, Afrika Kusini, Juni 19, 2024. (Xinhua/Zhang Yudong)
Helikopta ikiruka juu ya hafla ya kuapishwa kwa Rais Cyril Ramaphosa mjini Pretoria, Afrika Kusini, Juni 19, 2024. (Xinhua/Zhang Yudong)
Cyril Ramaphosa (Kulshoto) na mke wake wakihudhuria hafla ya kuapishwa kwake mjini Pretoria, Afrika Kusini, Juni 19, 2024. (Xinhua/Zhang Yudong)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma