

Lugha Nyingine
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa China na Nigeria wafanya mazungumzo mjini Beijing
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), akifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria Yusuf Maitama Tuggar, mjini Beijing, China, Juni 21, 2024. (Xinhua/Li Xiang)
BEIJING - Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi amefanya mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Nigeria Yusuf Maitama Tuggar mjini Beijing siku ya Ijumaa ambapo mawaziri hao wawili wa mambo ya nje pia walihudhuria mkutano wa kwanza wa wajumbe wote wa kamati kati ya serikali za China na Nigeria.
Kwenye mazungumzo kati ya viongozi hao wawili, Wang, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) amesema Nigeria ni nchi kubwa ya Afrika yenye ushawishi mkubwa na kwamba maendeleo mazuri ya uhusiano kati ya China na Nigeria yatakuwa mfano na mwongozo wa uhusiano kati ya China na Afrika.
China ingependa kujiunga pamoja na Nigeria kuwa ndugu wema wa kusaidiana , washirika wazuri wa kufanya ushirikiano wa kunufaishana, marafiki wazuri wa kutetea haki na usawa, na washirika wazuri wa kulinda amani na utulivu, amesema Wang, huku akiongeza kuwa nchi hizo mbili zitafanya kazi pamoja ili kupata maendeleo na ustawishaji, na kuinua uhusiano kati ya China na Nigeria na China na Afrika kwenye ngazi mpya.
Kwa upande wake Tuggar amesema Nigeria itaendelea kushikilia kithabiti kanuni ya kuwepo kwa China moja na inatarajia kuimarisha mawasiliano kwenye ngazi ya juu, kuzidisha uratibu wa kimkakati na kufanya ushirikiano wa karibu wenye manufaa halisi na China.
"Nigeria ingependa kuungana mkono na China ili kuunganisha nchi za Kusini, kudumisha ushirikiano wa pande nyingi, na kulinda haki na usawa," amesema.
Pande hizo mbili pia zimebadilishana maoni ya kina kuhusu ushirikiano kati ya China na Afrika na kukubaliana kufanya juhudi za pamoja katika kuhimiza mkutano mpya wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika kupata mafanikio mengi, mkutano ambao utakafanyika China msimu ujao wa mpukutiko.
Akihudhuria mkutano wa kwanza wa wajumbe wote wa kamati kati ya serikali za nchi hizo mbili, Wang amebainisha kuwa, kamati hiyo imekuwa mstari wa mbele kwenye ushirikiano kati ya China na Afrika katika kuhimiza ushirikiano wenye manufaa halisi tangu kuanzishwa kwake zaidi ya miaka mitatu iliyopita.
Tuggar amesifu sana matokeo ya mkutano huo wa kwanza, na kueleza nia ya kuendelea kuzidisha hali ya kuaminiana na China na kusukuma matokeo zaidi kwenye ushirikiano katika sekta mbalimbali.
Baada ya mkutano huo, pande hizo mbili zilitoa taarifa ya pamoja ya mkutano wa kwanza wa wajumbe wote wa kamati hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), na Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria Yusuf Maitama Tuggar, wakihudhuria mkutano wa kwanza wa wajumbe wote wa Kamati kati ya Serikali za China na Nigeria, mjini Beijing, China. Juni 21, 2024. (Xinhua/Li Xiang)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma