

Lugha Nyingine
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo aweka jiwe la msingi kwa mradi wa barabara za mzunguko zinazojengwa na China
Malori na bango vikionekana kwenye hafla ya kuweka jiwe la msingi kwa mradi wa barabara za mzunguko mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Juni 22, 2024. (Xinhua/Shi Yu)
KINSHASA - Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Felix Tshisekedi ameweka jiwe la msingi siku ya Jumamosi kwa mradi wa ujenzi wa barabara za mzunguko za Mji wa Kinshasa, moja ya miradi ya miundombinu ya kipaumbele ndani ya miradi ya ushirikiano wa "rasilimali kwa miradi" kati ya DRC na China.
Kwenye hafla hiyo iliyohudhuriwa na watu wa hadhi za juu, akiwemo Waziri Mkuu Judith Tuluka Suminwa, Rais Tshisekedi aliyeendesha greda mwenyewe amezindua ujenzi wa mradi huo.
Amesema "amehakikishiwa" na mbinu za Wachina huku akitamani uwepo wa ushirikiano wa aina mbalimbali na wa pande zote kati ya nchi hizo mbili.
Kwa Alexis Gisaro Muvuni, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Miundombinu na Kazi za Umma wa DRC, mradi huo unaashiria "hatua mpya" ya ushirikiano kati ya DRC na China ambayo inaimarisha muunganisho wa barabara za DRC na miradi mbalimbali ya miundombinu.
Mradi huo utavuka wilaya nne za Kinshasa, ambazo zinaishi wakazi zaidi ya milioni 17, huku barabara tisa zinazopenya zikiunganishwa na njia nne za makutano, ambazo zitasaidia kupunguza msongamano wa magari.
Zhao Bin, Balozi wa China nchini DRC, akitoa shukrani zake kwa uungaji mkono wa DRC kwa miradi ya ushirikiano wa "rasilimali kwa miradi", amesema mradi huo ni kama "alama mpya" ya Kinshasa na "ishara mpya" ya ushirikiano kati ya China na DRC katika sekta ya miundombinu.
Balozi Zhao Bin amesema, tangu ziara ya rais Tshisekedi nchini China mwezi Mei 2023, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili umekuwa ukiongezeka kwa kasi katika pande zote, Kituo cha Utamaduni na Sanaa cha Afrika ya Kati, ambacho ni msaada kutoka kwa serikali ya China kitakamilika, na kongamano la uwekezaji lililopangwa kufanyika Agosti.
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Felix Tshisekedi (Kulia) akipungia mkono watu katika mji mkuu wa DRC Kinshasa, Juni 22, 2024. (Xinhua/Shi Yu)
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Felix Tshisekedi akiendesha greda kwenye hafla ya kuweka jiwe la msingi kwa mradi wa barabara za mzunguko katika mji mkuu wa DRC, Kinshasa mnamo Juni 22, 2024. (Xinhua/Shi Yu)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma