

Lugha Nyingine
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania kufundisha wanahabari Kiswahili bila malipo
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nchini Tanzania kinatarajia kutoa mafunzo bila malipo kwa wanahabari kuhusu matumizi ya Kiswahili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Huduma kwa Umma ya Chuo hicho mwishoni mwa wiki siku ya Jumamosi, mafunzo hayo yanatarajiwa kufanyika kwa siku tano kuanzia leo Juni 24 hadi 28, na kutolewa na Taasisi ya Taaluma ya Kiswahili kwa kushirikiana na Kitengo cha Mafunzo Endelevu chuoni hapo.
Taarifa hiyo imesema walengwa wa mafunzo hayo ni wanahabari, watangazaji, wahariri, maofisa habari na uhusiano wa serikali na sekta binafsi kutoka vituo vya runinga, redio, magazeti na blogu za Kiswahili.
Lengo kuu la kutoa mafunzo hayo ni kukuza stadi ya matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika tasnia ya habari ili waandishi waimarike katika uandishi wao.
Pia mafunzo hayo yatalenga matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika uandishi, uhusiano wa vyombo vya habari na maendeleo ya Kiswahili na umuhimu wa ushirikiano wa vyombo vya habari na asasi za Kiswahili.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma