Rais wa Kenya awatuma maafisa 400 wa polisi nchini Haiti kukabiliana na ghasia za magenge

(CRI Online) Juni 25, 2024

Rais William Ruto wa Kenya ametangaza kundi la kwanza la maafisa 400 wa polisi watakaotumwa Haiti kupambana na ghasia za magenge.

Katika shughuli ya kuwaaga maofisa hao iliyofanyika mjini Nairobi, Rais Ruto alikabidhi bendera ya Kenya kwa maafisa ambao watashiriki katika Operesheni ya Kimataifa ya Kulinda Usalama nchini Haiti.

Ujumbe huu uliidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Oktoba 2, 2023 chini ya Azimio 2699.

Kutumwa kwa maofisa hao wa polisi kulikabiliwa na ucheleweshaji na changamoto kadhaa za kisheria, ikiwemo kutangazwa kuwa ni haramu na Mahakama Kuu ya Kenya. Licha ya vizuizi hivi, kundi hilo linatazamiwa kuondoka kuelekea Haiti siku ya Jumanne.

Inspekta Jenerali wa Polisi wa Kenya Japhet Koome amemteua msaidizi mkuu wa polisi Godfrey Otunge kuwa kamanda mpya wa zaidi ya maafisa 2,500 wa polisi wanaohusika katika operesheni hiyo nchini Haiti.

Wiki iliyopita, Kenya ilifikia makubaliano na serikali ya Haiti juu ya utaratibu wa ushiriki wa maofisa hao wa usalama, wanaoweza kukabiliwa na upinzani mkali wa magenge yenye silaha ambayo yanadhibiti mji mkuu wa Haiti.

Polisi zaidi ya 1,000 wa Kenya wataungana na timu nyingine za kimataifa nchini Haiti kushughulikia ghasia za magenge.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha