Kenya, UNHCR zazindua kituo cha kubadilishana taarifa za wakimbizi

(CRI Online) Juni 25, 2024

Serikali ya Kenya, kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) imezindua Kituo cha Rasilimali cha Wakimbizi ili kuendeleza utafiti na kubadilishana maarifa juu ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na vita, majanga ya asili na matatizo ya kiuchumi katika nchi zao.

Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi, maafisa wakuu wa serikali, wafanyakazi na wanafunzi walishiriki katika uzinduzi wa kituo hicho kitakachokuwa na makao yake katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Kwa mujibu wa Bw. Grandi, uzinduzi wa kituo hicho utaongeza juhudi za Kenya na jumuiya ya kimataifa kutafuta mifano endelevu ya kusimamia wakimbizi na wanaotafuta hifadhi katika nchi walizopokelewa.

Kituo hicho pia kitatoa jukwaa kwa watunga sera, watafiti, na watendaji wa masuala ya kibinadamu kuchunguza njia mpya za kuhimiza wakimbizi kujumuishwa na jamii zinazowapokea wakati msaada kutoka nje unapozidi kupungua.

Ameongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa ajira, na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe ni sababu za wimbi la wakimbizi na wanaotafuta hifadhi katika kanda hiyo, na kwamba utawala bora, uwajibikaji, na ongezeko la uchumi linalounga mkono watu maskini vinaweza kutoa ahueni.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha