Rais wa Kenya ayaelezea maandamano ya mitaani kuwa ya uhaini, jeshi latumwa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 26, 2024

NAIROBI - Rais wa Kenya William Ruto ameyaelezea maandamano ya mitaani yaliyofanyika siku ya Jumanne nchini humo kuwa ni uhaini, akibainisha kuwa serikali yake hivi karibuni itatoa mwitikio wa haraka kwa hali hiyo ambapo waandamanaji walivunja vizuizi vya usalama katika jengo la bunge la Kenya mjini Nairobi, na kuvamia jengo hilo saa chache baada ya wabunge kupitisha mswada wenye utata wa kuongeza ushuru.

Akilihutubia taifa kwa njia ya televisheni, Ruto amesema serikali imekusanya rasilimali zake zote ili kuhakikisha hali hiyo haitokei tena "kwa gharama yoyote ile."

Ameviagiza vyombo vya usalama kutumia njia zote zinazowezekana kuzuia vitisho vyovyote kwa usalama wa taifa.

"Inawezekana kwamba wahalifu waliosababisha majanga kwa watu wasio na hatia na kuvipa changamoto vyombo vyetu vya usalama huenda wakaendelea na tabia hii," amesema, akiongeza kuwa wapangaji, wafadhili na wachochezi wa maandamano hayo hawataachwa huru.

Kauli hizo za Ruto zimekuja saa chache baada ya waandamanaji takriban watano kuuawa kwa kupigwa risasi na wengine zaidi ya 150 kujeruhiwa huku maandamano yakizuka nchini kote kwa wiki ya pili mfululizo kupinga mswada mpya wa kutoza ushuru.

Waandamanaji hao wamekuwa wakikusanyika katika miji mbalimbali nchini Kenya, ukiwemo mji mkuu Nairobi, ambako wamevamia maeneo yenye ulinzi mkali ili kuingia katika Bunge la Taifa na lile la Seneti, wakiharibu mali na kuandamana hadi kwenye majengo hayo licha ya polisi kufyatua risasi hewani.

Kwenye hotuba yake hiyo, Rais Ruto amesema kuwa serikali haitavumilia uhalifu uliofanyika kwa kisingizio cha demokrasia. “Serikali italinda taifa na vitisho vyovyote kwa usalama wa taifa ni vitisho kwa nchi na vitashughulikiwa,” amesema.

Vikosi vya Jeshi la Ulinzi la Kenya vilitumwa siku ya Jumanne kuunga mkono Jeshi la Huduma ya Kitaifa la Polisi katika kukabiliana na hali ya dharura ya usalama iliyosababishwa na maandamano hayo ya ghasia yanayoendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi, Aden Duale Waziri wa Ulinzi wa Kenya, amesema.

Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta ametoa wito wa kujizuia na kufanya mazungumzo, akibainisha kuwa amehuzunishwa na vifo vya watu vilivyosababishwa na maandamano hayo.

Kenyatta amewaomba viongozi waliochaguliwa kusikiliza kero za wananchi, akitoa wito wa kujizuia na kuwataka viongozi "kuonyesha kujizuia na kufanya mambo sahihi kwa kuwasikiliza wananchi na kutokuwa dhidi yao."

Wabunge hao Jumanne asubuhi walipitisha muswada huo wenye utata wa mambo ya fedha wa Mwaka 2024, wakitaka kuongeza shilingi bilioni 346.7 (dola bilioni 2.67 za Marekani), kwa hatua kama vile kuongeza tozo ya maendeleo ya reli kutoka asilimia 1.5 hadi asilimia 2.5 na tozo ya tamko la kuagiza bidhaa nje ya nchi kutoka asilimia 2.5. hadi asilimia 3.5.

Wabunge hao pia wameanzisha ushuru wa kiikolojia kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje kama simu janja na vifaa vya kielektroniki, wakibainisha kuwa mwishowe huishia kuwa taka za kielektroniki zinazoharibu mazingira.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha