

Lugha Nyingine
Watano wauawa huku maandamano ya kupinga muswada wa fedha yakienea Kenya, Rais Ruto atangaza kutosaini muswada huo
Polisi wa kupambana na ghasia wakitawanya waandamanaji kwenye maandamano ya kupinga ongezeko la kodi katikati mwa jiji la Nairobi, Kenya, Juni 25, 2024. (Xinhua/Wang Guansen)
NAIROBI – Waandamanaji takriban watano wameuawa kwa kupigwa risasi na wengine zaidi ya 150 kujeruhiwa nchini Kenya siku ya Jumanne wakati maandamano yakizuka kote nchini humo kwa wiki ya pili mfululizo kupinga hatua mpya za kutoza ushuru zilizopendekezwa na serikali ya Rais William Ruto ingawa jana siku ya Jumatano Rais Ruto ametangaza kuwa serikali yake imeacha mapendekezo ya kuongeza ushuru, ambayo yamezua maandamano hayo ya nchi nzima tangu Juni 18 wakati mswada wa sheria ya fedha uliposomwa kwa mara ya kwanza bungeni.
Waandamanaji hao, kwa mamia yao, wamekuwa wakikusanyika katika miji mbalimbali nchini humo, ukiwemo mji mkuu, Nairobi.
Jijini Nairobi, waandamanaji takriban wanne wameuawa walipovamia majengo ya bunge, saa chache baada ya wabunge kupitisha muswada wa sheria hiyo tata ya fedha inayolenga kuongeza ushuru, huku mtu wa kwanza akipigwa risasi mtaani katika mji mkuu huo.
Waandamanaji hao walivamia sehemu zenye ulinzi mkali majira ya saa 9.00 alasiri (saa za Nairobi) ili kuingia katika Bunge la Taifa na lile la Seneti. Sehemu ya jengo hilo imechomwa moto na waandamanaji hao wenye hasira, ambao wengi wao walikuwa wakiimba nyimbo za kuipinga serikali.
"Walisema hatutaingia bungeni lakini tupo hapa. Wananchi wana nguvu," alifoka mwandamanaji ndani ya Bunge.
Wabunge wa nchi hiyo Jumanne asubuhi walipitisha muswada huo wenye utata wa mambo ya fedha wa Mwaka 2024, wakitaka kuongeza shilingi bilioni 346.7 (dola bilioni 2.67 za Marekani), kwa hatua kama vile kuongeza tozo ya maendeleo ya reli kutoka asilimia 1.5 hadi asilimia 2.5 na tozo ya kuagiza bidhaa nje ya nchi kutoka asilimia 2.5 hadi asilimia 3.5 na hatua nyingine mbalimbali za tozo na ushuru.
Hata hivyo, Rais wa Kenya William Ruto jana Jumatano ametangaza kutosaini mswada huo wa kuongeza ushuru wakati maandamano hayo makali yakiendelea, huku akitangaza pia hatua za kubana matumizi.
Akizungumza kwenye mkutano na wanahabari jijini Nairobi, Ruto amesema serikali yake itaweka mikakati ya kubana matumizi baada ya kuondoa hatua hizo za kuongeza ushuru.
"Ninaelekeza hatua za haraka za kubana matumizi ili kupunguza matumizi. Bajeti ya shughuli za rais itapunguzwa, pamoja na usafiri na ununuzi wa magari," amesema, huku akiongeza kuwa hatua hizi zitatumika kwa kaunti na wizara pia.
"Baada ya kupitishwa kwa mswada huo, nchi imeshuhudia maandamano na uharibifu wa taasisi za kikatiba. Nikisikiliza kwa makini watu wa Kenya, ambao wamesema kwa sauti kubwa kwamba hawataki chochote kinachohusiana na Mswada huu wa Fedha wa 2024, nakubali na kwa hivyo sitautia saini, na hatimaye utaondolewa," Ruto amesema.
Polisi wa kupambana na ghasia wakitawanya waandamanaji kwenye maandamano ya kupinga ongezeko la kodi katikati mwa jiji la Nairobi, Kenya, Juni 25, 2024. (Xinhua/Wang Guansen)
Waandamanaji wakiandamana kupinga ongezeko la ushuru katikati mwa jiji la Nairobi, Kenya, Juni 25, 2024. (Xinhua/Wang Guansen)
Polisi wa kutuliza ghasia wakizuia waandamanaji kwenye maandamano ya kupinga ongezeko la ushuru katika jiji la Nairobi, Kenya, Juni 25, 2024. (Xinhua/Wang Guansen)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma