

Lugha Nyingine
China yaitaka Israel itekeleze wajibu wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza
UMOJA WA MATAIFA - China siku ya Jumanne imeitaka Israel kutimiza wajibu wake chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu na kutii wito wa jumuiya ya kimataifa wa kuhakikisha misaada ya kibinadamu kuingia kwenye Ukanda wa Gaza kwa haraka na usalama.
Katika hotuba yake kwenye kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, likiwemo suala la Palestina, mjumbe wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa Fu Cong ameangazia janga kubwa la kibinadamu mjini Gaza, linalosababishwa uhaba mkubwa wa mahitaji muhimu na hali mbaya ya kiafya.
Amebainisha kuwa "mamilioni ya watu wanahangaika na njaa, magonjwa, maumivu, na kukata tamaa," akielezea hali hiyo kuwa janga la kibinadamu linasababishwa na mtu na inakwenda kinyume na sheria za kimataifa.
Fu amesema kuwa Gaza imekuwa katika vizuizini kwa miezi tisa, huku watu zaidi ya milioni 2 wakiishi katika "gereza la wazi" bila maji ya kutosha, umeme, chakula, dawa na mafuta.
Amekosoa kufungwa kwa kivuko cha Rafah kutokana na operesheni za kijeshi za Israel, ambako kumeacha maelfu ya malori yaliyosafirisha vifaa vya kibinadamu yakisubiri kwenye foleni ndefu.
"Njia zilizopo za vivuko vya mipakani hazitosheleza mahitaji ya msaada wa kibinadamu," Fu amesema, akisisitiza kuwa njia za usafiri wa nchi kavu ni muhimu katika kupanua ufikiaji wa kibinadamu.
Fu pia amezungumzia kizuizi cha usambazaji wa mahitaji ya kibinadamu na changamoto zinazokabili wafanyakazi wa kibinadamu, ambao hukutana na hali nyingi ngumu na shutuma zisizo na sababu.
Amelaani mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya vituo vya mashirika ya kibinadamu na kubainisha kuwa wafanyakazi zaidi ya 200 wa kibinadamu wamekufa katika vita hivyo, akiielezea hali hiyo kuwa ambayo "haijawahi kutokea katika historia na ya kushtua."
Amesema, azimio namba 2720 iliyopitishwa na baraza hilo ililenga kupanua ufikiaji wa kibinadamu, lakini utekelezaji wake umeshindwa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma