

Lugha Nyingine
Maafisa wa China na Ethiopia watoa wito wa kukumbatia ustaarabu mbalimbali kwa ajili ya Dunia yenye amani na bora
ADDIS ABABA - Maafisa wa China na Ethiopia kwenye mazungumzo ya ngazi ya juu, yaliyopewa jina la "Mihadhara kuhusu Ustaarabu," yaliyofanyika Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, siku ya Jumamosi wamesisitiza haja ya kuheshimu na kukumbatia anuai ya staarabu ili kuendeleza kuishi pamoja kwa amani, uhusiano kati ya watu na maendeleo kote duniani.
Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha zaidi mawasiliano na ushirikiano wa jamii za kiraia kati ya China na Ethiopia.
Akizungumza kwenye mazungumzo hayo, makamu mkuu wa Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya China kwa ajili ya Mawasiliano ya Kimataifa, Li Jun, amesema ni muhimu kutetea na kueneza maadili ya pamoja ya binadamu ili kuendeleza kuishi pamoja kwa amani kati ya ustaarabu na watu mbalimbali duniani.
"Tunapaswa kuheshimu anuai ya ustaarabu ili kuhimiza maelewano, kuhamasisha tofauti za utamaduni kulingana na usawa na heshima, na kukataa kiburi na chuki, ambavyo vimethibitishwa kuwa ni vikwazo vikubwa kwa mawasiliano na kufunzana kati ya ustaarabu na utamaduni tofauti," Li amesema.
Kwa mujibu wa Li, serikali ya China inaunga mkono kithabiti juhudi za Waethiopia na wengine kurithi na kuendeleza tamaduni zao huku wakichagua kwa kujiamulia njia ya maendeleo inayoendana na hali halisi za nchi zao. Amesema, China inapenda kufanya mazungumzo zaidi kuhusu ustaarabu, mawasiliano katika utamaduni na uzoefu wa utawala wa nchi.
Yonas Adaye, kamishna wa Mazungumzo ya Kitaifa ya Ethiopia, amesema katika mazungumzo hayo kwamba mazungumzo juu ya ustaarabu ni muhimu kwa kudumisha amani na maendeleo ya Dunia kupitia mawasiliano na ushirikiano kati ya tamaduni tofauti.
Akibainisha kuwa China inahimiza amani ya dunia kupitia ushirikiano na mshikamano, Adaye amesisitiza haja ya kuendeleza mazungumzo na kushirikiana kati ya ustaarabu katika kukabiliana na migogoro inayoongezeka kati ya nchi za Dunia.
Mazungumzo hayo ya ngazi ya juu yamekuja baada ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mazungumzo kati ya Ustaarabu iliyopendekezwa na China, ambayo iliteuliwa kuwa Juni 10 ya kila mwaka katika Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma