

Lugha Nyingine
China yahimiza vikundi vyote vyenye silaha nchini DRC kuweka silaha chini mara moja
Naibu Mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa, Geng Shuang, katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichojadili suala la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) siku ya Jumatatu amesema kuwa, China inahimiza makundi yote yenye silaha nchini DRC kuweka chini silaha mara moja na kuondoka kwenye maeneo wanayoyakalia.
Geng Shuang amesisitiza kuwa, jumuiya ya kimataifa inapaswa kuhimiza kusimamisha mapigano na kuzuia vurugu za makundi yenye silaha katika DRC.
Amesema kuwa katika kipindi cha miezi mitatu pekee iliyopita, raia zaidi ya 500 wameuawa na makundi hayo yenye silaha, na watu zaidi ya milioni 7.3 wamelazimika kuyakimbia makazi yao.
Amesema, Jumuiya ya kimataifa inapaswa kuheshimu mamlaka, uhuru na ukamilifu wa ardhi ya nchi ya DRC, kutoa usaidizi wa kujenga kwa DRC katika kudumisha usalama na utulivu na kuboresha hali ya kibinadamu, na kuharakisha suluhu ya mapema kwa suala la mashariki mwa DRC.
Geng Shuang amesema kuwa, ni muhimu kuhimiza kutulia kwa hali ya kikanda haraka kadri iwezavyo. Amesema, hivi karibuni, kumekuwa na kuongezeka kwa migogoro na kutokuelewana kati ya nchi za kikanda kuhusu suala la mashariki mwa DRC.
“China inatoa wito kwa nchi husika kudumisha utulivu na kujizua, kufikia suluhu ya hali ya kutoelewana kupitia mazungumzo, na kuepuka kutumia njia za kijeshi” amesema.
Geng amesema China inapongeza uwezeshaji wa Angola kwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje kati ya DRC na Rwanda mwezi Machi, na inatarajia nchi na mashirika ya kikanda kutoa mchango mkubwa zaidi katika kuendeleza mchakato wa Luanda na mchakato wa Nairobi.
Geng Shuang amesema kuwa kujiondoa kwa Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Kuleta Utulivu DRC (MONUSCO) inabidi kuendelezwe kwa namna ya utaratibu.
Amesema, katika hatua inayofuata, mfumo wa Umoja wa Mataifa unapaswa kulisaidia Jimbo la Kivu Kusini kujenga na kuimarisha amani, na MONUSCO inapaswa kudumisha mawasiliano na serikali ya DRC, ili kuendeleza mchakato wa kujiondoa kwa namna salama na yenye utaratibu.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma