

Lugha Nyingine
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa China na Thailanda wafanya mkutano wa pili wa mfumokazi wa mashauriano
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), na mwenzake wa Thailand Maris Sangiampongsa wakifanya mazungumzo na kuongoza kwa pamoja mkutano wa pili wa Mfumokazi wa Mashauriano kati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa China na Thailand, mjini Beijing, China, Julai 9, 2024. (Xinhua/Yue Yuewei)
BEIJING - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi na mwenzake wa Thailand Maris Sangiampongsa wamefanya mazungumzo na kuongoza kwa pamoja mkutano wa pili wa Mfumokazi wa Mashauriano kati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa China na Thailand, mjini Beijing siku ya Jumanne.
Huku akibainisha kuwa ujenzi wa jumuiya ya China na Thailand yenye mustakabali wa pamoja umesonga mbele kwa matokeo yenye manufaa, Wang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) amesema China inaichukulia Thailand kama mwenzi wa kuaminika na nguvu ya kulinda amani na utulivu wa kanda.
Wang amesema mwaka ujao utakuwa wa maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Thailand, akitoa wito kwa pande zote mbili kuimarisha ushirikiano wa kimkakati wa pande zote.
Amesema China na Thailand zinapaswa kushughulikia matatizo katika Reli ya China-Laos-Thailand, kuboresha kiwango cha muunganisho, kuimarisha ushirikiano wa usalama wa utekelezaji wa sheria na kukabiliana kwa pamoja na uhalifu unaovuka mipaka, kama vile kucheza kamari mtandaoni na utapeli wa kielektroniki.
Wang pia ametoa wito kwa pande zote mbili kutumia vyema sera ya kusameheana visa, kupanua mawasiliano ya kitamaduni, kuimarisha mawasiliano ya kirafiki kati ya vijana, na kuendeleza urafiki kati ya China na Thailand kutoka kizazi hadi kizazi.
Kwa upande wake Sangiampongsa amesema serikali ya Thailand inatilia maanani sana uhusiano wake na China na itaendelea kufuata bila kuyumba sera ya kuwepo kwa China moja.
“Thailand inapenda kushirikiana na China kuandaa vizuri shughuli za kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Thailand na China, kuongeza mawasiliano ya ngazi ya juu, kuzidisha mawasiliano kati ya watu na ya kitamaduni, na kuimarisha ushirikiano wenye manufaa halisi katika uchumi wa kidijitali, magari yanayotumia umeme, nishati mbadala, utalii na nyanja zingine ili kunufaisha watu wa nchi hizo mbili,” Sangiampongsa amesema.
Mawaziri hao wawili pia wamebadilishana maoni kuhusu ushirikiano wa kikanda katika Asia Mashariki, ushirikiano wa Lancang-Mekong na suala la Myanmar.
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), na mwenzake wa Thailand Maris Sangiampongsa wakifanya mazungumzo na kuongoza kwa pamoja mkutano wa pili wa Mfumokazi wa Mashauriano kati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa China na Thailand, mjini Beijing, China, Julai 9, 2024. (Xinhua/Yue Yuewei)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma