China yasema NATO haipaswi kuitumia China kuhalalisha jaribio lake la kuvuruga mienendo ya kikanda

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 10, 2024

BEIJING - Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Lin Jian siku ya Jumanne amesema China inakataa kithabiti kauli za kukashifiwa na lawama zinazotolewa na Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO) dhidi ya China, akiongeza kuwa NATO haipaswi kuitumia China kuhalalisha kujiingiza eneo la Asia-Pasifiki na kujaribu kuvuruga mienendo ya kikanda.

Lin ameyasema hayo kwenye mkutano na wanahabari alipoulizwa kutoa maoni yake kuhusu kauli za hivi karibuni za Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg kuhusu China.

Habari zinasema, Stoltenberg alisema kwenye mkutano na waandishi wa habari wa kabla ya mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi wanachama wa NATO kwamba ushirikiano wa kimataifa wa NATO utakuwa moja ya agenda za Mkutano huo wa kilele.

Alisema kuwa "kama tunavyoona nchini Ukraine, usalama wetu si wa kikanda, ni wa kimataifa" na kwamba ni muhimu "kushirikiana kwa karibu na marafiki zetu katika eneo la Indo-Pasifiki." Kwamba NATO itajadili ushirikiano juu ya Ukraine na mada nyingine pamoja na Australia, Jamhuri ya Korea, Japan na New Zealand ili kuzizuia Russia, Iran, DPRK (Jamhuri wa Kidemokrasia ya Watu wa Korea) na China.

Lin amesema ikiwa ni mabaki ya Vita Baridi na chombo kikubwa zaidi cha kijeshi duniani, NATO inajidai kuwa jumuiya ya ulinzi wa kikanda, lakini kwa upande mwingine inaendelea kuvuka nje ya mipaka yake, ikipanua mamlaka yake, ikichochea mapambano na kujifanya kama mnyanyasaji kwenye jukwaa la Dunia.

"Kile kinachoitwa usalama wa NATO mara nyingi kimejengwa juu ya ukosefu wa usalama wa wengine, na kile inachofanya kinaweka Dunia na kanda nyingine katika hatari kubwa ya usalama," Lin amesema.

Akibainisha kuwa China ni nguvu kwa ajili ya amani ya dunia, inatoa mchango kwa ajili ya maendeleo ya dunia na inalinda utaratibu wa kimataifa, Lin amesema msimamo wa China kutopendelea upande wote na wa haki na mchango wake wa kiujenzi katika mgogoro wa Ukraine na masuala ya kimataifa na ya kikanda unatambuliwa na jumuiya ya kimataifa.

China inaitaka NATO kuwa na mtazamo sahihi wa China, kuachana na mawazo yake ya Vita Baridi na mbinu ya kupata manufaa kwa kukandamiza wengine, kuacha kuleta uvumi wa hofu ya usalama na kujitengenezea maadui wa kufikirika, kuacha kuunda vilabu mahsusi kwa jina la ulinzi wa pamoja, na kutoa mchango wa kiujenzi kwa amani, utulivu na maendeleo ya kimataifa, Lin amesema.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Renato Lu)

Picha