Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za EAC waeleza wasiwasi kuhusu hali ya kibinadamu na usalama mashariki mwa DRC

(CRI Online) Julai 10, 2024

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wameeleza wasiwasi wao kuhusu kuzorota kwa hali ya kibinadamu na usalama katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Taarifa iliyotolewa na jumuiya hiyo Jumatatu wiki hii baada ya mawaziri hao kukutana huko Zanzibar, Tanzania, imesema mawaziri hao wamepongeza hali ya sasa ya kusimamishwa kwa vita nchini DRC na kupendekeza hali hiyo kudumishwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mawaziri hao wamejadili hali ya amani, usalama na uhusiano kati ya nchi wanachama, na mchakato wa mafungamano ya EAC. Pia wamesisitiza kuwa mchakato wa kisiasa ni njia inayofaa kufikia amani na usalama endelevu mashariki mwa DRC.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Renato Lu)

Picha