China na Afrika kutafuta ushirikiano zaidi kati ya serikali za mitaa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 11, 2024

GUANGZHOU - Viongozi wa China na Afrika wamesisitiza kuongeza ushirikiano kati ya serikali za mitaa za pande hizo mbili kwenye mkutano wa 5 wa Baraza la Ushirikiano wa Serikali za Mitaa kati ya China na Afrika uliofanyika katika Mji wa Guangzhou, Kusini mwa China.

Wajumbe takriban 350 walihudhuria mkutano wa baraza hilo, wakiwemo viongozi wa kisiasa, viongozi na wakuu wa mashirika kutoka China na Afrika. Wahudhuriaji hao wamekubaliana kuimarisha ushirikiano kati ya serikali za mitaa, kuhimiza kunufaika kwa pamoja na uzoefu wa utawala, kukabiliana na matatizo kwa pamoja, na kufanya ushirikiano wa kunufaishana ili kupata maendeleo kwa pamoja.

Christian Ntsay, Waziri Mkuu wa Madagascar, amesema kwenye mkutano wa baraza hilo kwamba, kuimarisha ushirikiano wa serikali za mitaa ni muhimu kwa maendeleo endelevu. Amesema jukwaa hilo linatoa fursa kwa nchi za Afrika kutafuta fursa za maendeleo kwa kuimarisha ushirikiano na urafiki kati ya watu wa China na Afrika.

Kwenye mkutano wa baraza hilo, Ntsay alishuhudia kusainiwa kwa makubaliano yenye nia ya kuimarisha urafiki, mawasiliano na ushirikiano kati ya Mji wa Foshan huko Guangdong na Mji wa Sambava nchini Madagascar.

Takwimu zilizotolewa na Shirika la Urafiki wa Watu wa China kwa Nchi za Nje zinaonyesha kuwa mikoa, maeneo na miji 28 nchini China imeanzisha uhusiano 166 wa miji-dada na wenzao katika nchi 35 za Afrika. Miongoni mwao, Guangzhou imeanzisha uhusiano wa miji-dada na bandari-dada na miji 10 na bandari 5 za Afrika, mtawalia.

Zhao Baogang, naibu meya wa Mji wa Weihai wa Mkoa wa Shandong mashariki mwa China, amesema, katika miezi mitano ya kwanza ya mwaka huu, bidhaa za Weihai za kuagizwa na kuuzwa barani Afrika ziliongezeka kwa asilimia 73.2 na kwamba mji huo umeanzisha kampuni za biashara katika nchi 22 za Afrika, zinazohusisha sekta za kilimo, nishati na afya.

Shirika la Urafiki wa Watu wa China kwa Nchi za Nje na serikali ya mkoa wa Guangdong kwa pamoja zimeandaa mkutano huo wa mwaka huu wa baraza hilo la Ushirikiano wa Serikali za Mitaa kati ya China na Afrika, ambalo lilianzishwa rasmi Mwaka 2012. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha