

Lugha Nyingine
Mradi wa ujenzi wa kisasa wa barabara wa DRC unaojengwa na China wawekewa jiwe la msingi
Alexis Gisaro Muvuni, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Miundombinu na Kazi za Umma wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, akiendesha greda la kubeba mchanga kuzindua mradi wa ukarabati na ujenzi wa kisasa wa barabara ya Mbuji Mayi-Nguba, ambayo ni sehemu ya Barabara ya Taifa ya N1, huko Nguba, Jimbo la Lualaba, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), tarehe 10 Julai 2024. (Xinhua/Shi Yu)
KOLWEZI, DR Congo – Hafla ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa ukarabati na ujenzi wa kisasa wa barabara ya Mbuji Mayi-Nguba, ambayo ni sehemu ya Barabara ya Taifa ya N1, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imefanyika siku ya Jumatano katika kijiji cha Nguba, jimbo la kusini mashariki la Lualaba, ikiwa ni sehemu ya ushirikiano wa "rasilimali kwa miradi" kati ya China na DRC.
Kwenye hafla hiyo, Alexis Gisaro Muvuni, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Miundombinu na Kazi za Umma wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, akiendesha greda kubeba mchanga, amezindua mwenyewe mradi huo wa barabara inayounganisha Kinshasa, mji mkuu wa DRC, na Lubumbashi, mji kitovu cha uchumi wa nchi hiyo.
“Pale barabara inapokwenda maendeleo yanafuata,” amesema Muvuni huku akipongeza mbinu thabiti na weledi ulioonyeshwa na upande wa China.
Miradi mingi ya miundombinu iliyozinduliwa hivi karibuni chini ya kifurushi cha miradi ya ushirikiano, ikiwa ni pamoja na mradi wa barabara za mzunguko huko Kinshasa, imepangwa kutoa mchango mkubwa kwa jamii za wenyeji.
Mradi huo, wenye urefu wa takriban kilomita 900, unaonyesha urafiki kati ya China na DRC huku ukifungua matarajio mapya ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, amesema Pang Long, mkurugenzi mkuu wa Kampuni ya Miundombinu ya China na Kongo, akiwakilisha upande wa China katika miradi hiyo.
Pia ameahidi ushirikiano wa karibu na DRC ili mradi huo wa hali ya juu ukamilike haraka iwezekanavyo na kunufaisha wananchi wa DRC.
Alexis Gisaro Muvuni, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Miundombinu na Kazi za Umma wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, akizungumza kwenye hafla ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa ukarabati na ujenzi wa kisasa wa barabara ya Mbuji Mayi-Nguba, ambayo ni sehemu ya Barabara ya Taifa ya N1, huko Nguba, Jimbo la Lualaba, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), tarehe 10 Julai 2024. (Xinhua/Shi Yu)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma