

Lugha Nyingine
Wasanii wa Namibia wahamasisha uhifadhi wa wanyamapori kupitia maonyesho ya Sanaa
Msanii akichora mchoro huku watu wakitazama kazi za sanaa kwenye maonyesho yenye kichwa cha "Tuokoe dhidi ya Kutoweka" huko Windhoek, Namibia, Julai 11, 2024. (Picha na Ndalimpinga Iita/Xinhua)
WINDHOEK - Wasanii wa Namibia wanachukua msimamo wa kulinda wanyamapori kupitia maonyesho yaliyopewa jina la "Tuokoe dhidi ya Kutoweka," kwenye Jumba la Sanaa la Omba huko Windhoek, mji mkuu wa Namibia ambayo yamefunguliwa Juni 18 na yataendelea hadi Julai 14, yakiwa na mkusanyiko wa kazi za Sanaa zaidi ya 70, ikiwa ni pamoja na mikato, picha za kuchora na vinyago.
Kazi hizo za Sanaa zimeundwa na wasanii wenyeji Jeremia Haihambo na Nghiwilepo Tuhafeni, na zote zikiwa na picha za faru na wanyamapori wengine walio hatarini kutoweka.
Kwa mujibu wa Haihambo, kazi hizo za sanaa, zilizobuniwa mwaka zaidi ya mmoja uliopita, zinatumika kama kikumbushaji cha haja ya dharura ya kukabiliana na ujangili wa faru na biashara haramu ya wanyamapori, ambayo inaleta changamoto kubwa kwa taifa hilo la kusini mwa Afrika.
“Ujangili unaoendelea umetuhamasisha kushikamana kutetea uhai na haki ya jamii ya mwisho iliyobakia ya faru katika nchi yetu na Afrika kwa ujumla,” amesema Haihambo Alhamisi.
Namibia imekuwa ikikabiliwa na hasara ya wanyamapori wake kutokana na tishio linaloendelea la uwindaji haramu wa faru, hasa wanyama wanaothaminiwa sana kama vile pangolin.
Pohamba Shifeta, Waziri wa Mazingira, Misitu na Utalii wa Namibia, amesema kuwa idadi ya faru waliouawa iliongezeka kutoka 79 mwaka 2022 hadi 83 mwaka 2023 na kwamba kulikuwa na ongezeko kubwa la pangolin waliokamatwa mwaka 2023 kufuatia kupungua Mwaka 2022.
"Sanaa inafanya kazi kama wito wenye nguvu kwa ajili ya utunzaji na ulinzi wa wanyamapori," Haihambo amesema.
Wakati huo huo, wasanii hao wanalenga kutumia kikamilifu sanaa ili kubadilisha mitazamo na tabia juu ya mazingira asilia. Kwa Tuhafeni, maonyesho hayo pia yanalenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa faru kwa uchumi wa nchi.
Mapato yatakayopatikana kutokana na maonyesho hayo yatatolewa kwa Mfuko wa Okoa Faru (Save the Rhino Trust), ambao ni shirika la Namibia lisilo la faida, na pia yataunga mkono masomo ya wasanii katika chuo cha sanaa cha nchini humo.
Wasanii wakichora michoro kwenye maonyesho yenye kichwa cha "Tuokoe dhidi ya Kutoweka" huko Windhoek, Namibia, Julai 11, 2024. (Picha na Ndalimpinga Iita/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma