

Lugha Nyingine
Mpango wazinduliwa ili kukuza mabadilishano kati ya watoto wa China na Afrika
BEIJING - Mradi unaolenga kuhimiza mawasiliano kati ya watoto wa China na Afrika umeanzishwa Beijing siku ya Jumapili ambapo hafla ya makaribisho iliyofanyika kwenye Kituo cha Kitaifa cha Watoto cha China imeshuhudia makumi ya watoto kutoka Namibia, Afrika Kusini, Somalia, Uganda na Jamhuri ya Afrika ya Kati wakikusanyika pamoja na watoto wa China.
Shughuli mbalimbali ziliandaliwa kwa ajili ya watoto, ikiwa ni pamoja na michezo, ngoma na michezo ya Wushu, na darasa la kuchora picha kwa pamoja.
Katika eneo la mali ya urithi wa kitamaduni usioshikika wa kituo hicho, watoto wameguswa na mvuto wa utamaduni wa jadi wa China walipokuwa wakitengeneza mifuko yenye harufu nzuri na vikaragosi vya kivuli.
Huang Xiaowei, naibu mkuu wa Shirikisho Kuu la Wanawake la China, amesema watoto wanabeba mustakabali wa siku za baadaye na matumaini ya China na Afrika, na kwamba mawasiliano kati ya watoto yataongeza uhai mpya katika kuendeleza urafiki kati ya China na Afrika.
Shughuli za mradi huo zinaandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya China na Shirikisho Kuu la Wanawake la China. Katika siku sita zijazo, watoto hao wa China na wa nchi tano za Afrika pia watatembelea Makumbusho ya Kasri la Mfalme ya Beijing, pamoja na maeneo ya mabaki ya kale ya kitamaduni katika Mkoa wa Henan, katikati ya China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma