UNHCR yatahadharisha kuwa mgogoro nchini Sudan unachochea janga la kibinadamu nchini Sudan Kusini

(CRI Online) Julai 16, 2024

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limetahadharisha katika utafiti wa majaribio uliotolewa Jumatatu kwamba mgogoro unaoendelea nchini Sudan unachochea hali ya kibinadamu kuwa mbaya zaidi nchini Sudan Kusini kwa wakimbizi na jamii zinazowahifadhi.

Utafiti huo wa kijamii na kiuchumi unaonesha kuwa wale wanaolazimika kukimbilia Sudan Kusini mara nyingi hufikia katika maeneo ya vijijini yenye huduma duni za kimsingi, viwango vya juu vya ukosefu wa ajira, ukosefu wa fursa za elimu, miundombinu duni, na makazi yenye msongamano mkubwa wa watu.

Mwakilishi wa UNHCR nchini Sudan Kusini, Marie-Helene Verney amesema mamilioni ya Wasudan Kusini wanaishi chini ya mstari wa umaskini, na vita vya Sudan vinaathiri vibaya uchumi wa Sudan Kusini.

Matokeo ya Utafiti huo wa UNHCR kwa Watu Waliolazimika Kukimbia Makazi Yao uliofanyika kati ya Aprili na Disemba 2023 kwa kaya 3,100 nchini Sudan Kusini yanaonesha kuwa wakimbizi na jamii zinazowahifadhi wanakabiliwa na changamoto zinazofanana ambazo zinazidisha hatari za ulinzi na kupunguza fursa za kujitegemea.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha