Sudan Kusini yazindua kampeni ya chanjo dhidi ya malaria katika majimbo sita

(CRI Online) Julai 17, 2024

Sudan Kusini imezindua kampeni ya chanjo dhidi ya malaria ya R21 siku ya Jumanne katika kaunti 28 za majimbo sita ya nchi hiyo.

Akiongea mjini Juba Waziri wa Afya wa nchi hiyo Yolanda Awel Deng, amesema chanjo hiyo italenga watoto kuanzia umri wa miezi 18 hadi miaka mitano katika kaunti 28 za majimbo ya Bahr el Ghazal Kaskazini, Bahr el Ghazal Magharibi, Warrap, Ikweta ya Kati, Jonglei, na Ikweta Mashariki.

Waziri Deng amefafanua kuwa licha ya jitihada zinazoendelea, ugonjwa wa malaria unaendelea kuwa tishio kubwa kwa taifa hilo ambapo kila mwaka nchi hiyo inakabiliwa na wagonjwa wanaokadiriwa kufikia milioni 2.8 na vifo 6,680, ikimaanisha wagonjwa 7,630 na vifo 18 kila siku.

Uzinduzi wa kampeni hiyo ya chanjo umekuja baada ya serikali kupokea dozi 645,000 za chanjo dhidi ya malaria ya R21 Mei 31 kutoka Muungano wa Chanjo Duniani, Gavi.

Waziri huyo amebainisha kuwa majimbo yaliyolengwa yamechaguliwa kutokana na kiwango kikubwa cha maambukizi ya malaria, na kuongeza kuwa wizara yake inalenga kuchanja watoto wapatao 265,897 katika awamu ya kwanza ya kampeni hiyo ya chanjo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha