

Lugha Nyingine
Meli ya Hospitali ya Kikosi cha Wanajeshi wa Majini cha China “Peace Ark” yawasili Tanzania kwa ajili ya ziara na kutoa huduma za matibabu
Meli ya hospitali ya kikosi cha wanajeshi wa majini cha Jeshi la Ukombozi wa Umma la China (PLA) ikiwasili kwenye bandari ya Dar es Salaam, Tanzania, Julai 16 kwa saa za Tanzania. (Picha na Gui Xinhua/Kutoka tovuti ya Wizara ya Ulinzi ya China)
Meli ya hospitali ya kikosi cha wanajeshi wa majini cha Jeshi la Ukombozi wa Umma la China (PLA), “Peace Ark”, iliyo katika “Jukumu la Masikilizano 2024” imewasili bandari ya Dar es Salaam siku ya Jumanne, tarehe 16, na kuanza ziara ya kirafiki ya siku saba ya kituo chake cha pili cha jukumu lake, Tanzania.
Meli hiyo tayari imeanza kutoa huduma za matibabu ya kibinadamu na hii ni mara ya tatu kwa meli hiyo ya “Peace Ark” kufanya ziara Tanzania.
Siku hiyo majira ya saa nne asubuhi, meli hiyo ya “Peace Ark” ilitia nanga taratibu kwenye bandari ya Dar es Salaam.
Mkuu wa Huduma za Matibabu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Meja Jenerali Amri Mwani na baadhi ya maofisa wa jeshi na wa kisiasa, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian na wafanyakazi wengine wa ubalozi, wenyeji, wachina wanaoishi Tanzania pamoja na wawakilishi wa kampuni za China zalizowekeza nchini humo waliikaribisha meli hiyo kwenye gati la bandari.
Katika ziara yake hiyo, meli ya “Peace Ark” itatoa huduma za upimaji afya na matibabu kwenye jukwaa lake kuu, na pia itapeleka timu 10 za madaktari kwenye hospitali, mitaa na shule mbalimbali kutoa huduma hiyo, na kufanya shughuli za pamoja za huduma za upimaji afya na matibabu, mabadilishano ya kitaalamu, na shughuli nyinginezo na upande wa Tanzania.
Meli hiyo ya “Peace Ark” iliwahi kutembelea Tanzania na kutoa huduma za matibabu mnamo mwaka 2010 na 2017. Mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 60 tangu China na Tanzania zilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia, ambapo ziara ya meli hiyo itatoa mchango katika kuimarisha zaidi urafiki wa jadi na kuzidisha mabadilishano na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma