

Lugha Nyingine
Umoja wa Afrika watoa wito mafungamano ya bara kwenye mkutano wa uratibu wa katikati ya mwaka
Picha hii iliyopigwa tarehe 21 Julai 2024 ikionyesha Mkutano wa 6 wa Uratibu wa Katikati ya Mwaka wa Umoja wa Afrika (AU) ukifanyika mjini Accra, Ghana. (Picha na Seth/Xinhua)
ACCRA - Umoja wa Afrika (AU) umefungua mkutano wake wa sita wa uratibu wa katikati ya mwaka siku ya Jumapili wenye kaulimbiu isemayo "Elimisha na Ipe Ustadi Afrika kwa Karne ya 21" huko Accra, mji mkuu wa Ghana, ukitoa wito wa amani na mshikamano wa bara hilo.
Mkutano huo umekutanisha pamoja AU, Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda (RECs), na nchi wanachama wa AU, miongoni mwa baadhi ya wengine.
Katika hotuba yake, Mwenyekiti wa Kamati ya AU Moussa Faki Mahamat amesisitiza kuwa Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika (AfCFTA) limetoa mchango mkubwa katika kuendeleza mafungamano ya bara hilo.
"AfCFTA ina wajibu wa kuwa chachu inayochochea mageuzi ya kimuundo ambayo, hatimaye, yatawezesha kuundwa kwa utajiri, kupitia kuboresha usimamizi wa uchumi, kuhamasisha mambo ya fedha na mtaji watu," Faki amesema.
Mwenyekiti huyo pia ametoa wito kwa nchi za Afrika kuongeza uwezo wa AfCFTA ili kuifanya kuwa injini ya ukuaji na uchumi anuwai, na kuongeza biashara ndani ya bara hilo.
Kwa upande wake Rais wa Ghana Nana Addo Dankwa Akufo-Addo, ambaye alifungua mkutano huo, amesema baadhi ya sehemu barani Afrika bado zinakumbwa na migogoro, ukosefu wa utulivu, na ghasia ambazo zinazuia maendeleo na kuwa tishio kwa usalama mpana wa bara hilo.
Rais huyo ametoa wito kwa viongozi wenzake wa Afrika kufanya kazi kwa bidii kutafuta suluhu la migogoro mingi barani humo.
AU ilianzisha mkutano wake huo wa uratibu wa katikati ya mwaka Mwaka 2017 kama jukwaa kuu la kuoanisha kazi za AU na RECs na kuratibu utekelezaji wa ajenda ya mafungamano ya bara hilo.
Rais wa Ghana Nana Addo Dankwa Akufo-Addo akitoa hotuba kwenye ufunguzi wa Mkutano wa 6 wa Uratibu wa Katikati ya Mwaka wa Umoja wa Afrika (AU) mjini Accra, Ghana. (Picha na Seth/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma