Kampuni ya huduma za intaneti nchini Zimbabwe yaingia ubia na kampuni ya China Telecom ili kutoa huduma za mtandao wa kasi

(CRI Online) Julai 26, 2024

Kampuni inayotoa huduma za mtandao wa intaneti nchini Zimbabwe Dandemutande imezindua rasmi makubaliano ya ushirikiano na kampuni ya mawasiliano ya simu ya China Telecom siku ya Alhamisi ili kutoa huduma ya intaneti yenye kasi kwa wafanyabiashara wa China nchini humo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo Never Ncube amesema, ushirikiano huo unawezesha wafanyabiashara wa China nchini Zimbabwe kupata huduma ya intaneti ya kasi na ya kuaminika kutoka Zimbabwe hadi China.

Amesema ushirikiano wa kampuni hiyo na kampuni ya China Telecom unahakikisha kuwa kuna njia maalum iliyotengwa hususan kwa wafanyabiashara wa China, na hivyo kupunguza ucheleweshaji wa shughuli za kibiashara.

Meneja Mkuu wa kampuni ya China Telecom nchini Afrika Kusini Zhang Guangzhu amesema, kampuni hiyo daima imejikita katika kuboresha muunganisho wa intaneti na mawasiliano barani Afrika.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha