

Lugha Nyingine
Idadi ya watu waliofariki kutokana na mkanyagano katika mji mkuu wa DRC yaongezeka hadi kufikia 9
Picha hii iliyopigwa kwa kutumia simu ya mkononi tarehe 27 Julai 2024 ikionyesha watu wakishiriki kwenye tamasha katika Uwanja wa Mashujaa, Stade des Martyrs huko Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) (Str/Xinhua)
KINSHASA – Watu takriban tisa, wakiwemo wanawake wawili, wamethibitishwa kufariki dunia kwenye mkanyagano katika tamasha la muziki lililofanyika siku ya Jumamosi mjini Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), amesema Waziri wa Afya wa DRC Roger Kamba, matukio kadhaa ya watu kujeruhiwa vibaya yameripotiwa pia katika ajali hiyo iliyotokea kwenye tamasha la mwanamuziki Mike Kalambayi katika ukumbi wa Uwanja wa Mashujaa, Stade des Martyrs.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya DRC ilisema siku hiyo ya Jumamosi jioni kwamba, Kutokana na maagizo ya Waziri Mkuu wa DRC Judith Suminwa Tuluka, mkutano wa kujadili janga uliitishwa.
Ukiwa na viti 80,000, Uwanja wa Mashujaa, Stade de Martyrs ni moja ya viwanja vikubwa zaidi nchini humo. Vyanzo vya usalama vimesema kuwa uwanja huo ulikuwa umejaa kupita uwezo wake huo wakati mkanyagano huo ulipotokea.
Serikali ya manispaa ya Mji wa Kinshasa imetangaza mwishoni mwa Jumamosi kuanzisha uchunguzi wa tukio hilo.
Oktoba Mwaka 2022, watu 11, wakiwemo maafisa wawili wa polisi, waliuawa kwenye mkanyagano katika tamasha la mwimbaji wa DRC Fally Ipupa kwenye uwanja huo huo.
Wakati huo huo, Naibu Waziri Mkuu wa DRC anayeshughulikia Mambo ya Ndani Jacquemain Shabani amesema jana Jumapili kwamba shughuli zote zisizo za kimichezo zitasitishwa kwenye viwanja vya michezo katika mji huo wa Kinshasa hadi itakapotoa taarifa nyingine, ikiwa ni siku moja tu baada ya kutokea kwa mkanyagano huo.
“Kipaumbele chetu ni kuweka watu wetu salama, hatuwezi kuvumilia shughuli za matamasha zinazohatarisha maisha ya wananchi wenzetu, shughuli zote hizi zimesitishwa kwa muda, waandaaji watalazimika kuzingatia maeneo mengine yenye usalama zaidi kwa ajili ya shughuli hizo,” amesisitiza Shabani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma