

Lugha Nyingine
Maonyesho ya China na Nchi za Asia Kusini yahitimishwa kwa kusainiwa mikataba ya biashara yenye thamani ya dola bilioni 1.12
Muonyeshaji bidhaa wa Pakistan (Kushoto) akitambulisha zulia kwa watembeleaji maonyesho kwenye Banda la Asia Kusini katika Maonyesho ya 8 ya China na Nchi za Asia Kusini huko Kunming, Mkoa wa Yunnan, kusini-magharibi mwa China, Julai 26, 2024. (Xinhua/Wang Jingyi)
KUNMING - Maonyesho ya nane ya China na Nchi za Asia Kusini yamehitimishwa jana Jumapili, huku mikataba ya biashara ya ndani na nje ya China yenye thamani ya jumla ya yuan zaidi ya bilioni 8 (dola karibu bilioni 1.12 za Kimarekani) ikiwa imetiwa saini, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na waandaaji wa maonyesho hayo.
Kwenye maonyesho hayo yaliyofanyika Kunming, mji mkuu wa Mkoa wa Yunnan kusini-magharibi mwa China, jumla ya mauzo yote ya mtandaoni na nje ya mtandao yalizidi Yuan milioni 500.
Maonyesho hayo ya siku sita yana kumbi 15 za maonyesho zenye mambo mbalimbali yakiwemo ya teknolojia ya usanifu majengo, viwanda vya uzalishaji, nishati ya kijani na kilimo cha kisasa.
Maonyesho hayo ya mwaka huu yameshuhudia ushiriki kutoka nchi, kanda na mashirika ya kimataifa 82, huku kukiwa na kampuni zaidi ya 2,000 zilizoonyesha bidhaa. Karibu nusu ya kampuni hizi zinatoka nchi za nje, zikiwa ni pamoja na nchi zote za Asia Kusini na Asia Kusini-Mashariki.
Maonyesho hayo yalifanyika kwa mara ya kwanza mjini Kunming Mwaka 2013, mwaka huo huo ambao China ilitangaza Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja. Tangu kuanzishwa kwake, maonyesho hayo yamehudumia kampuni zaidi ya 18,000 za ndani na nje ya China, yamekuza biashara yenye thamani ya dola za Kimarekani zaidi ya bilioni 100, na kuwezesha kutiwa saini kwa miradi zaidi ya 3,000.
Yakiwa yameandaliwa kwa pamoja na Wizara ya Biashara ya China na serikali ya mkoa wa Yunnan, maonyesho hayo ni moja ya shughuli muhimu zaidi za mwaka huu kwa mawasiliano ya kiuchumi na kibiashara kati ya China na nchi za Asia Kusini.
Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa thamani ya biashara kati ya China na nchi za Asia Kusini yalifikia dola za Marekani karibu bilioni 200 Mwaka 2023, kiasi ambacho ni mara mbili ya kilichorekodiwa Mwaka 2013.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma